TARSI, CTI watoa mafunzo kwa madereva kupunguza ajali

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 06:06 PM Jun 17 2025
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa TARSI, Maliki Balongo.

Katika juhudi za kupunguza ajali za barabarani, Taasisi ya Mpango wa Usalama Barabarani (TARSI) kwa kushirikiana na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), wameendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo madereva wanaofanya kazi za usafirishaji viwandani.

Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia ongezeko la ajali nyingi za barabarani, ambapo sababu kubwa zikitajwa kuwa ni uzembe na kutozingatia sheria za usalama barabarani.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo ya siku mbili yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TARSI, Maliki Balongo, alisema wameamua kuungana na CTI kuwapatia madereva elimu hiyo kutokana na umuhimu wa sekta ya viwanda katika kutumia usafirishaji wa bidhaa kwa magari kwenda maeneo mbalimbali nchini.

Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwakumbusha madereva mambo mbalimbali ya usalama barabarani ambayo baadhi yao wamekuwa wakiyasahau, hali inayosababisha ajali na madhara mengine.

Kwa upande wake, Ofisa Wanachama na Huduma kutoka CTI, Annette Temu, alisema moja ya majukumu ya shirikisho hilo ni kuhakikisha wanachama wake wanaongezewa ujuzi, ikiwemo kwa madereva wanaohudumu katika sekta ya viwanda.

Amesema mafunzo hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwa madereva pamoja na maofisa usafirishaji kwa kuwa yamewasaidia kujifunza mambo mapya pamoja na kukumbushwa yale waliyoyasahau, na kwamba yataendelea kufanyika mara kwa mara kwa sababu pia kuna sheria mpya zinazotarajiwa kuanza kutumika.

Mmoja wa madereva waliopatiwa mafunzo hayo kutoka Kampuni ya Azam, Said Mselemo, alisema yameongeza maarifa katika kazi zao za kila siku, huku akishauri elimu hiyo ifikishwe pia kwa madereva wengine wengi.

Amesema mafunzo hayo yamewasaidia kutambua mambo muhimu ya usalama barabarani ambayo awali hawakuwa wanayafahamu kikamilifu au walikuwa wameshayasahau, hivyo sasa wanaamini watakuwa mabalozi wa kufuata sheria barabarani.

Naye dereva mwingine, Muhamed Jaa, alisema madereva wengi wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea, hivyo mafunzo kama hayo yana umuhimu mkubwa kwao, kwani yanawasaidia kuwajengea uelewa na nidhamu katika utendaji kazi wao wa kila siku.

Alishauri TARSI kutanua wigo wa mafunzo hayo kwa kuwahusisha pia watumishi wa idara za utawala ili wanapopata mafunzo kama hayo wapate ruhusa kwa urahisi na kuongeza ufanisi katika sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa nchi.