Kipara adakwa na polisi tuhuma kupanga njama kumuua mama yake

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 06:29 PM Jun 17 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Seven Kipara (38), Mkazi wa Ipwizi Wilaya ya Mbeya kwa tuhuma za kupanga njama ya mauaji ya mama yake mzazi, Kweji Lugembe (75), na kusababisha kujeruhiwa kwa mtoto wa miaka minne, Sinzo Jifwalo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga, amesema tukio hilo lilitokea Juni 13, 2025 majira ya saa sita  usiku, katika eneo la Ipwizi, ambapo mtuhumiwa Tabi Deus anadaiwa kufyatua risasi katika dirisha la nyumba  na kumjeruhi mtoto Jifwalo ambaye alikuwa amelala pamoja na bibi yake.

“Mtoto huyo alijeruhiwa kwenye bega la kushoto na mdomoni kwa risasi za Shot Gun, baada ya wauaji waliokodishwa kukosea shabaha yao,” alisema Kamanda Kuzaga.

Kwa mujibu wa Kamanda Kuzaga, uchunguzi wa awali umebaini kuwa tukio hilo linahusishwa na imani za kishirikina, ambapo inadaiwa Seven Kipara na mdogo wake Jifaru Kipara walimtuhumu mama yao, Kweji Lugembe, kuwa mshirikina anayehusika na vifo vya  watoto  wao na ndugu zao.

Amesema katika  harakati za kutekeleza njama hizo, watuhumiwa walikodi watu wawili kutoka mkoani Lindi  ambao ni Tabi Deus (39) na mtuhumiwa mwingine aitwaye Shija  kwa makubaliano ya kuwalipa Shilingi milioni tano ili wamuue mama yao.

Kamanda Kuzaga ameeleza kuwa  wauaji hao walifika Mbalizi Juni 8, 2025 na kulala katika nyumba ya wageni hadi Juni 10, wakisubiri maelekezo kutoka kwa mwenyeji wao Kipara walielekezwa mazingira ya nyumbani kwa mama huyo, na hatimaye Juni 13, 2025, walitekeleza jaribio la mauaji.

Baada ya tukio, Jeshi la Polisi lilianzisha msako na kufanikiwa kuwakamata  Kipara na Deus ambaye   alikutwa na bastola ya kutengenezwa kienyeji isiyo na namba na risasi mbili za Shot Gun ndani ya mkoba wake.

Akiwa mikononi mwa Polisi  Juni  15, 2025,  Deus aliwaongoza askari hadi kwenye maficho  ya mtuhumiwa Shija, wakati wa operesheni hiyo katika eneo la korongo, Shija alijaribu kukimbia, akakaidi amri halali ya kusimama, na ndipo alipodungwa risasi mguuni na kukamatw, alikimbizwa Hospitali Teule ya Ifisi kwa matibabu lakini alifariki dunia.

“Jeshi la Polisi  linaendelea  na  uchunguzi na msako dhidi ya watu wengine walioshiriki katika njama hiyo ya uhalifu tunatoa rai kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi, “ amesema Kamanda Kuzaga.