Wadau wa Sekta Binafsi kupitia Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) wamekutana leo jijini Dar es Salaam kuchambua na kutoa maoni kuhusu bajeti ya serikali ya mwaka 2025/2026, wakisisitiza umuhimu wa mageuzi ya mfumo wa kodi ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa TPSF, Raphael Maganga, alisema bajeti ya mwaka huu inalenga kuinua uchumi wa Watanzania, hivyo ni muhimu kwa sekta binafsi kuipitia kwa kina na kutoa mapendekezo yatakayoiwezesha serikali kuiboresha zaidi.
“Mkutano huu ni sehemu ya majadiliano ya kitaifa. Tunapitia bajeti ili kuangalia maeneo muhimu yanayogusa biashara na uwekezaji. Ikiwa mfumo wa kodi utaboreshwa, wafanyabiashara watakuwa huru zaidi kukuza mitaji yao,” alisema Maganga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Oasis Financial Services Limited, ambaye pia ni mshauri wa masuala ya kodi, Stambuli Myovela, alisema kuwa mjadala huo unalenga kuchambua athari chanya na changamoto ndani ya bajeti.
“Faida ambayo haijagawanywa ikitozwa kodi inaweza kudhoofisha mitaji ya kampuni, hivyo tunashauri kuwe na msimamo unaoendana na mazingira halisi ya biashara,” alisema Myovela.
Aliongeza kuwa bajeti ya mwaka huu imeonyesha juhudi za kulinda viwanda vya ndani kwa kupunguza kodi kwa bidhaa zinazozalishwa nchini ikilinganishwa na zile zinazoagizwa kutoka nje, hatua itakayochochea uzalishaji wa ndani.
Kwa mujibu wa TPSF, bajeti ya mwaka 2025/2026 yenye jumla ya zaidi ya Shilingi trilioni 56, inahitaji mfumo madhubuti wa ukusanyaji kodi ili kufanikisha malengo yake bila kuongeza mzigo kwa walipakodi.
“Tukiboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato, serikali haitalazimika kukopa mara kwa mara, hali itakayopunguza deni la taifa,” aliongeza Maganga.
Katika mkutano huo pia alikuwepo mdau mwingine wa sekta binafsi, John Wananja, ambaye alisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi katika utekelezaji wa bajeti hiyo.
Naye Dkt Mwajuma Hamza ambaye ni Mkurugenzi wa chemba ya wanawake wafanya biashara, amesema kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa yale maeneo ambayo tunaona yanachangamoto serikali iingilie kati.
Kwa upande wetu kuna maeneo ambayo Serikali imetufurahisha na mengine tutaomba Serikali itusaidie hasa katika maswala ya biashara na maswala nishati safi ya kupikia ambayo tutaomba kodi ipunguzwe
"Zaidi ya asilimia 70 ya wanawake walishio vijini nibwakulima hivyo tunaipongeza serikali kwa kuipa kipaumbele katika swala la kilimo"
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED