Kijana anusurika kifo baada ya kujitupa baharini

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 05:03 PM Jun 17 2025
Kijana anusurika kifo baada ya kujitupa baharini

Kijana mmoja amenusurika kufa baada ya kujitupa baharini akiwa katika boti ya Zan Fast Ferries iliyokuwa ikitoka Pemba kuelekea Unguja, majira ya saa nane mchana wa leo, Juni 17, 2025.

Kijana huyo aliyetambulika kwa jina la Muhammed Shaib Saleh (35), mkazi wa Mbuyuni Pemba, alijirusha katikati ya mkondo wa bahari ya Nungwi wakati boti hiyo ikiendelea na safari yake.

Baada ya tukio hilo, mabaharia wa boti hiyo waliweza kumuokoa kwa haraka na kumkabidhi kwa askari wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano, huku hali yake ikiwa inaendelea vizuri.

Baadhi ya mashuhuda waliokuwemo ndani ya boti hiyo wamesema kuwa kabla ya kijana huyo kujitupa alikuwa akiuuliza mara kwa mara kama tayari wamefika eneo la Nungwi.

“Kijana hakuwa anaonekana kama ana matatizo ya akili, sijui alipatwa na nini hadi akachukua uamuzi wa kujitupa baharini,” amesema mmoja wa mashuhuda, Rashid Sultani.

Nahodha wa boti hiyo, Muhamed Khamis, akizungumza na Nipashe Digital, amesema walichukua hatua za haraka kwa kuzima injini ya boti na kurusha vifaa vya uokozi, ambapo zoezi hilo lilichukua takribani dakika 10 kumwokoa kijana huyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), Mtumwa Said, amesema uwepo wa vifaa vya kisasa vya uokozi umechangia kuokoa maisha ya kijana huyo.

Boti hiyo ya mwendo kasi ilikuwa imeondoka Bandari ya Mkoani, Pemba, majira ya saa saba mchana na huchukua wastani wa saa tatu kufika Bandari ya Malindi, Unguja.