Balozi Kingu aihakikishia Matembwe ushirikiano upatikanaji wa umeme Njombe

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:38 AM Jun 18 2025
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu (mbele) akikagua miundombinu ya usafirishaji umeme katika mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji wa Matembwe mkoani Njombe.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu (mbele) akikagua miundombinu ya usafirishaji umeme katika mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji wa Matembwe mkoani Njombe.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, ameihakikishia ushirikiano Kampuni ya Matembwe Village Company Limited ya mkoani Njombe ili kuiwezesha kuongeza upatikanaji wa umeme na kuwafikia wananchi wengi zaidi waishio maeneo hayo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu (katikati) akikagua miundombinu ya uzalishaji umeme katika mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji wa Matembwe Mkoani Njombe unaomilikiwa na Kampuni ya Matembwe Village Company Limited Juni 17, 2025 ambapo aliahidi kutoa ushirikiano kwa kampuni hiyo.Ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake katika mradi wa kuzalisha na kusambaza umeme wa Matembwe, uliopo katika Tarafa ya Lupembe, Wilaya ya Njombe, mkoani Njombe, Juni 17, 2025.

"Nimekagua mradi mzima kuanzia eneo la uzalishaji na nimetembelea baadhi ya wanufaika wa mradi ili kujionea uendeshaji wake, uwezo wake na namna ambavyo mradi huu unanufaisha wananchi katika kujiletea maendeleo," alifafanua Balozi Kingu.

Alisema ameridhishwa na namna mradi huo unavyofanya kazi na kusisitiza kuwa ipo haja ya kuongeza uzalishaji hasa ikizingatiwa kuwa vyanzo vya maji vya mradi huo vinatosheleza mahitaji.

Aidha, aliuahidi uongozi wa mradi kuwa Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) itaendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha uwezeshaji unaendelea ili kuleta tija zaidi kwa jamii.

"Kazi iliyofanyika hapa ni kubwa na inaridhisha. Ni wakati wenu sasa kujipanga vizuri kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme katika mradi huu ili walau mtoke kwenye kiwango mnachozalisha sasa cha kilowati 550 na muweze kuzalisha umeme mwingi zaidi kwa ajili ya kuinua shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa maeneo haya na nchi nzima kwa ujumla," alielekeza Balozi Kingu.

Pia aliwasisitiza wahusika kuendelea kutunza mazingira ili kuwezesha miradi hii kuwa endelevu sambamba na kuwajengea uwezo vijana wa vijiji vinavyonufaika na mradi huo katika usimamizi na uendeshaji wake.

"Vijana wanapaswa kutambua kuwa huu mradi ni wao. Walianzisha babu zao na sasa wao wenyewe wananufaika," alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Matembwe, Johannes Kamonga, alisema uhitaji wa umeme ni mkubwa hasa kipindi hiki ambacho viwanda vingi vinajengwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Aliipongeza REA kwa mchango mkubwa na kuomba uwezeshaji zaidi ili kuwezesha upanuzi wa mradi pamoja na kuunganisha wateja wengi zaidi.

Kamonga alieleza kuwa awali mradi ulianza kwa kuzalisha kilowati 120, lakini kutokana na ongezeko la mahitaji walilazimika kutafuta uwezeshwaji ili kuongeza uzalishaji pamoja na kuongeza idadi ya wanufaika.

"Tunaishukuru REA kwani imekuwa bega kwa bega nasi. Tulianza na vijiji viwili, lakini kwa uwezeshwaji kutoka REA sasa tunahudumia vijiji nane," alisema Kamonga.

Akifafanua kuhusu uwezeshaji wa mradi huo, Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage, alisema REA imechangia takriban shilingi bilioni moja kuuwezesha mradi huo, hatua ambayo imesababisha kuunganishwa kwa wateja 357 sawa na asilimia 16.18.

Alisema REA imewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kuzalisha na kusambaza umeme vijijini katika mikoa yote ya Tanzania Bara kwa lengo la kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma bora ya nishati, kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa, kuongeza ajira, kuongeza mapato ya serikali na kuboresha maisha ya Watanzania waishio vijijini.

Aidha, alieleza kuwa mradi huo wa Matembwe unatumia teknolojia ya kusambaza umeme kwa kutumia nyaya zinazopita ardhini, jambo linaloongeza usalama na kupunguza gharama za matengenezo.

"Kwa sasa REA ipo katika hatua ya kuongeza idadi ya kaya 95 kupitia mkataba wa ruzuku ya nyongeza ya fedha," alieleza Mhandisi Mwijage.

Aliongeza kuwa REA imefadhili miradi ya uzalishaji na usambazaji wa nishati vijijini inayotekelezwa na taasisi mbalimbali za Serikali na sekta binafsi kwa kutoa ruzuku, kuwezesha mikopo yenye masharti nafuu, pamoja na kuwajengea uwezo waendelezaji wa miradi husika. Miongoni mwa miradi hiyo ni huu wa Matembwe.

Mradi wa kuzalisha na kusambaza umeme wa Matembwe unaendeshwa na kusimamiwa na Kampuni ya Matembwe Village Company Ltd kwa kushirikiana na Serikali za Vijiji vya Matembwe, Yembela na Ikondo, ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.