Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga imepata Hati Safi kwa hesabu za mwaka wa fedha 2023/2024 ulioishia Juni 30, 2024.
Taarifa hiyo imetolewa Juni 11, 2025 na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Dk. Kalekwa Kasanga, wakati akiwasilisha ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2023/2024, katika kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo.
Dk. Kasanga alisema katika ukaguzi huo, ziliibuliwa hoja 52, ambapo hoja mbili zimefungwa na kubaki hoja 50 ambazo utekelezaji wake bado unaendelea.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukutaarifu kwamba kwa hesabu za mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni 2024, Halmashauri yako imepata Hati Safi,” alisema Dk. Kasanga.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Ibrahim Makana, ameipongeza halmashauri hiyo kwa kupata Hati Safi na kusimamia vyema rasilimali za umma.
Naye Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Mkoa wa Shinyanga, CPA Yusuph Mabwe, alisema utekelezaji wa mapendekezo ya hoja zilizobaki unapaswa kuongezewa kasi kwa kuwa ni hoja zinazotekelezeka.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, aliipongeza halmashauri hiyo kwa kupata Hati Safi pamoja na kufanikisha ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 106.
Aidha, Mtatiro alitoa maagizo kwa hoja 50 ambazo utekelezaji wake bado unaendelea, kwamba vielelezo vya kujibu hoja hizo viwe vimepatikana ndani ya siku saba. Pia alielekeza ifikapo Juni 18, Katibu Tawala wa Wilaya apange kikao maalum cha kupitia hoja hizo moja baada ya nyingine kwa kushirikisha wahusika wote.
Akijibu maagizo hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Dk. Kalekwa Kasanga, alisema atahakikisha maagizo yote yanatekelezwa ipasavyo na kuongeza kuwa suala la kufunga hoja zilizobaki limepewa kipaumbele.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED