Jumla ya watoto 1,630 waliokuwa wakijihusisha na ajira za watoto au waliokuwa katika hatari ya kuingia kwenye ajira hizo wameokolewa visiwani Zanzibar.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, kati ya watoto hao, 1,629 wanatoka Pemba huku mtoto mmoja akitokea Unguja. Watoto hao walikuwa wakifanya shughuli mbalimbali zikiwemo kuvunja kokoto, kupara samaki na kujihusisha na shughuli za uvuvi.
Shariff ametoa taarifa hiyo leo, Juni 11, 2025, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mwanakwerekwe, Zanzibar, kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ajira za Watoto Duniani ambayo hufanyika Juni 12 kila mwaka.
Amesema kati ya watoto hao, wavulana walikuwa 1,127 na wasichana 502.
Aidha, Waziri Shariff amesema kuwa wizara yake imefanikiwa kuwakamata watoto wa kike 86 walioingia Zanzibar mwezi Aprili mwaka huu, pamoja na watoto 90 mwezi Mei, wakiwemo wasichana 67 na wavulana 23 waliotoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara, ambao waliletwa kwa lengo la kufanyakazi za majumbani na kwenye migahawa.
Licha ya mikakati mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kupinga ajira za watoto, Waziri Shariff amesema bado changamoto hiyo inaendelea kuwa kubwa duniani, huku akibainisha kuwa kwa mujibu wa takwimu za kimataifa, zaidi ya watoto milioni 160 ulimwenguni wanakadiriwa kuwa kwenye ajira za watoto.
Ameongeza kuwa Tanzania, kama mwanachama wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), nayo bado inakabiliwa na changamoto hiyo.
“Takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Novemba 2024 zinaonesha kuwa watoto milioni 5.1 wanajihusisha na ajira za watoto Tanzania Bara na Zanzibar,” amesema.
Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha inatokomeza kabisa tatizo hilo, sambamba na kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya ajira za watoto.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED