Wafanyabiashara 1,520 kurejea Soko la Kariakoo

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 05:38 PM May 28 2025
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila
Picha: Imani Nathaniel
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila

Serikali imethibitisha kuwa wafanyabiashara 1,520 waliokuwa awali Soko la Kariakoo watarejeshwa kuendelea na shughuli zao, huku 1,159 tayari wamesajiliwa kupitia mfumo wa kidigitali wa Tausi na wamesaini mikataba.

Mtendaji wa Shirika la Masoko la Kariakoo, Ashiraf Yusuph, amesema wafanyabiashara wamegawanywa katika makundi ya vizimba, wauzaji wa nafaka/viuatilifu na wapya. Kati ya vizimba 764, wafanyabiashara 627 (81%) tayari wako tayari kuanza.

Kwa waliokufa, taratibu za mirathi zitatekelezwa ndani ya mwezi mmoja, huku wafanyabiashara 99 wenye madeni wakitakiwa kulipa ndani ya siku 10.

Maboresho ya soko ni pamoja na kamera za ulinzi, maegesho, stoo, na huduma za kifedha kupitia benki. Ukarabati umefikia asilimia 98.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewataka wafanyabiashara ndogondogo kuondoa biashara zao mitaani kabla ya soko kufunguliwa rasmi mwezi Julai.