PURE Growth Fund kufungua maombi ya miradi ya Nishati Safi na Biashara za Kilimo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:48 PM May 28 2025
Mfuko wa Ufadhili wa Mradi wa PURE Growth Fund Wafungua Mlango wa Maombi na Mapendekezo ya Nishati Safi na Biashara za Kilimo nchini Tanzania
Picha: Mpigapicha Wetu
Mfuko wa Ufadhili wa Mradi wa PURE Growth Fund Wafungua Mlango wa Maombi na Mapendekezo ya Nishati Safi na Biashara za Kilimo nchini Tanzania

Taasisi ya Ubia wa Nishati Jadidifu na Ufanisi wa Nishati (REEEP) imetangaza kufunguliwa rasmi kwa awamu ya kwanza ya kupokea maombi na mapendekezo kupitia Mfuko wa PURE Growth Fund Tanzania. Huu ni mpango wa kimkakati unaolenga kuleta mageuzi katika matumizi yenye tija ya nishati mbadala kwenye mifumo ya kilimo cha chakula nchini Tanzania, sambamba na kufungua fursa mpya kwa uzalishaji mdogo na wa kati.

Kwa kuzingatia vipaumbele vya Taifa katika kuboresha ushindani kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo, kuongeza upatikanaji wa huduma za nishati ya kisasa vijijini, na kuongeza mchango wa nishati jadidifu hadi kufikia 75% ya uzalishaji wa nishati ifikapo mwaka 2030, Mfuko huu unalenga kukuza uhusiano kati ya sekta ya kilimo na nishati. Kwa mujibu wa Shirika la Chakula Duniani (FAO), sekta hizi mbili huajiri zaidi ya 70% ya watu wanaoishi Kusini mwa Jangwa la Sahara na kuchangia kati ya 20-30% ya Pato la Taifa. Hapa Tanzania, kilimo kinachangia asilimia 24.3 ya Pato la Taifa na kutoa ajira kwa asilimia 55 ya wananchi.

Dirisha la Kwanza la Ufadhili Lafunguliwa

Dirisha la kwanza la ufadhili chini ya Mfuko wa PURE Growth Fund litatoa mtaji wa motisha wa jumla ya EUR milioni 2.5 (sawa na zaidi ya shilingi bilioni 7.6). Kila kampuni itakuwa na nafasi ya kupata kiasi cha kuanzia EUR 250,000 hadi EUR 1,000,000 (sawa na shilingi milioni 760 hadi bilioni 3), pamoja na usaidizi wa kiufundi na msaada wa sera. Lengo ni kusaidia ukuaji endelevu wa kampuni ndogo na za kati katika sekta ya nishati safi na biashara za kilimo, ili ziweze kupanua shughuli zao, kuongeza faida, na kuimarisha msingi wa wateja wao.

Dirisha hili la maombi litabaki wazi hadi tarehe 1 Agosti 2025, na utekelezaji wa miradi utatarajiwa kuanza Januari 2026. Mpango huu unatekelezwa na REEEP kwa ufadhili wa Serikali ya Austria.

Elfriede Anna More, Naibu Mkurugenzi Mkuu na Mkuu wa Masuala ya Kimataifa ya Hali ya Hewa na Mazingira kutoka Jamhuri ya Austria alisema:

 ‘Austria inajivunia kuwa mfadhili wa kwanza wa Mfuko wa PURE Growth Fund—mpango wa mageuzi unaoonyesha dhamira yetu ya kukuza mabadiliko ya nishati barani Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.’

Merja Laakso, Mkurugenzi wa Mipango wa REEEP aliongeza:

 “Programu hii itaondoa vikwazo vinavyozuia sekta binafsi kusonga mbele, kwa kusaidia kuunganisha mifumo ya pamoja badala ya tu kusambaza teknolojia. Hii itasaidia kujenga soko imara na kuwezesha upatikanaji wa huduma na teknolojia endelevu kutoka kwa PURE Growth Fund.”


Kwa kuunganisha teknolojia za PURE Growth Fund kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo—kuanzia umwagiliaji, uvunaji, usindikaji, uhifadhi hadi usafirishaji—mfuko huu utasaidia kuongeza uzalishaji wa chakula, kupunguza upotevu, na kuimarisha uthabiti wa wakulima dhidi ya changamoto za hali ya hewa na kifedha. Aidha, utapunguza pengo lililopo kati ya sekta ya nishati na kilimo kwa kutoa motisha kwa huduma ambazo zinaongeza manufaa ya teknolojia hizo katika uzalishaji wa chakula.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa alisema:

 “Uzinduzi wa Mfuko wa PURE Growth Fund ni hatua kubwa kuelekea kuwezesha jamii zetu kupitia suluhisho la nishati jadidifu kwenye kilimo, hivyo kuongeza vipato na kuboresha maisha ya wananchi kote nchini.”

Eva Kelly, Mkurugenzi Mtendaji wa REEEP, alisisitiza kuwa Tanzania ndiyo nchi ya kwanza kunufaika na mpango huu:

 “Tuna furaha kuzindua PURE Growth Fund nchini Tanzania kama hatua ya kwanza. Tunaamini kuna fursa kubwa ya nishati mbadala kubadilisha mnyororo wa thamani wa kilimo katika nchi nyingi za Kusini mwa Dunia.”

Biashara ndogo na za kati zinazojihusisha na nishati safi pamoja na wajasiriamali wa kilimo waliopo Tanzania wanakaribishwa kutuma maombi ya ufadhili na usaidizi kupitia Mfuko wa PURE Growth Fund. Mwongozo wa maombi—ikiwa ni pamoja na vigezo vya kustahiki, vipaumbele vya ufadhili, na maelekezo ya namna ya kuwasilisha maombi—unapatikana kupitia tovuti rasmi ya REEEP: www.reeep.org