Bosi PURA aeleza umuhimu wa teknolojia katika ustawi wa tasnia ya petroli

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 04:42 PM May 28 2025
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Teknolojia Afrika uliofanyika Mei 27, 2025 Jijini Dar es Salaam.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Teknolojia Afrika uliofanyika Mei 27, 2025 Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni amesema ukuaji wa teknolojia una mchango mkubwa katika ustawi na ufanisi wa tasnia ya petroli.

Mhandisi Sangweni ameyasema hayo Mei 27, mwaka huu, wakati akifungua Mkutano wa Teknolojia Afrika Jijiji Dar es Salaam.

Mkutano huo ulioandaliwa na Jumuiya ya Wahandisi wa Petroli Tanzania kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wahandisi wa Petroli Kanda ya Afrika umeleta pamoja washiriki takriban 200 kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujadili maendeleo ya tasnia ya petroli na kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali.

Miongoni mwa maeneo hayo ni pamoja na teknolojia za kisasa zinazotumika katika shughuli zinazotekelezwa katika mnyororo wa thamani wa petroli kama vile kuzalisha, kuchakata na kusafirisha Rasilimali za petroli.

Akitilia mkazo matumizi ya teknolojia, Sangweni alieleza umuhimu wa kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi na uzoefu wa matumizi ya teknolojia za kisasa zinazotumika katika tasnia hii.

“Ni muhimu kuwaandaa vijana wetu na wataalamu wetu kuendana na teknolojia au mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea duniani” alisema Sangweni. 
 
Sangweni pia aligusia suala la matumizi ya akili mnemba katika kutekeleza majukumu wanayofanya wahandisi wa petroli na kuwataka wanajumuia hiyo kuendelea kujiongezea maarifa katika eneo hilo muhimu.