Serikali ya Lesotho yavutiwa na Tanzania kupiga hatua usambazaji umeme vijijini

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 02:02 PM May 28 2025
 Serikali ya Lesotho yavutiwa na Tanzania kupiga hatua usambazaji umeme vijijini
PICHA: THOBIAS MWANAKATWE
Serikali ya Lesotho yavutiwa na Tanzania kupiga hatua usambazaji umeme vijijini

SERIKALI ya Lesotho imeeleza kuvutiwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijiji (REA) kupiga hatua kubwa katika usambazaji wa nishati safi vijijini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Lesotho, Tankiso Phapano, alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na wataalum wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) akiwa ameambata na ujumbe wa wataalam wa sekta ya nishati nchini humo.

"Tumefuatilia kwa karibu katika suala la nishati, Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua na zilizofanikiwa kwa upana wake na tupo hapa leo hii kubadilishana uzoefu na kujifunza siri hii ya mafanikio iliyowafikisha hapa," alisema Phapano.

 Alipongeza jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi Tanzania. Akizungumzia hali ya usambazaji wa nishati maeneo ya vijijini nchini humo, Meneja Kitengo cha Umeme Vijijini (REU), Leloko Mokhutsoane, alisema kwa sasa linasimamiwa na kitengo katika Shirika la Umeme la Lethoso (LEC).

 Mokhutsoane, alisema kutokana na kusuasua ufanisi wa kitengo hicho na mahitaji ya nishati safi ya kupikia maeneo ya vijijini, nchi hiyo inakwenda kuanzisha Wakala wa Nishati Vijijini. "Hiki ni kitengo tu tena kinahusika na umeme peke yake na sio nishati kwa upana wake, kwa sasa nasi tunataka kuwa na Wakala wa Nishati Vijijini kama ilivyo Tanzania ili suala la nishati safi nalo liingie na tusijifungie kwenye umeme tu," alisema.

 Akizungumzia uendeshaji wa shughuli za REA nchini kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wake, Hassan Saidy, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Jones Olotu, alisema wakati ikianzishwa mwaka 2007 vijiji 506 pekee vilikuwa vimefikiwa na umeme kati ya 12,318 vilivyopo nchini.

 Olotu, alisema Tanzania Bara kuna vitongoji 64,359 kati ya hivyo, 33,657 sawa na asilimia 52.3 vimefikishiwa umeme. Alisema upelekaji umeme katika vitongoji 30,702 unaendelea, 7,736 vipo katika miradi inayoendelea kujengwa na 9,000 REA ipo katika hatua ya ununuzi wa wakandarasi na kutarajiwa kukamilika mwezi ujao.