Wakati wimbi la watoto wadogo kutumikishwa katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kufanya kazi linaendelea kushika kasi, baadhi ya wananchi wameiomba serikali kuchukua hatua madhubuti kukomesha hali hiyo. Wameitaka pia jamii kushirikiana katika kuhakikisha watoto hao wanarejea shuleni badala ya kutumika kwenye biashara za kutembeza bidhaa mitaani, zikiwemo mbogamboga, matunda, karanga na mayai.
Maoni hayo yametolewa na wananchi mbalimbali akiwemo Simbili Abdalah Makanyaga, Alex Mchopa na Yusuph Kuonewa, walipokuwa wakizungumza katika mahojiano maalum kuhusu mwenendo wa baadhi ya wazazi na walezi kuwatuma watoto kufanya biashara na kuwaacha bila elimu.
Katika maelezo yao, wananchi hao walibainisha kuwa sehemu kubwa ya watoto wanaotumikishwa katika kazi hizo ni wale wanaoishi na mama wa kambo.
"Kumekuwa na tabia ya baadhi ya wazazi na walezi—hasa mama wa kambo—kuwatuma watoto kufanya kazi ambazo ni za watu wazima, ikiwemo kuzungusha biashara mitaani kama vile kuuza mbogamboga, matunda, mayai na karanga," alieleza Simbili.
Aliongeza kuwa hali hiyo imeanza kuzoeleka ndani ya jamii kiasi cha watoto wengi kuacha shule kutokana na utoro wa mara kwa mara.
"Wapo watoto wengi wanaofanyishwa kazi hata siku za masomo. Hatimaye huacha shule kabisa na kukosa haki yao ya msingi ya elimu," alisisitiza.
Kwa upande wake, Alex Mchopa alikumbusha kuwa mzazi au mlezi ana jukumu la kuhakikisha mtoto anakua katika mazingira salama na yenye ulinzi katika kila nyanja ya maisha.
"Mzazi au mlezi ana wajibu wa kuhakikisha mtoto anakua kwa usawa—kimwili, kiakili, kihisia, kimaadili, kiimani na kijamii," alisema Mchopa.
Aliongeza kuwa jamii inapaswa kuzingatia malezi bora yanayomruhusu mtoto kucheza, kujifunza na kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazojenga ustawi wake.
"Malezi bora ni yale yanayojengwa kwa msingi wa upendo na udhibiti wa tabia, huku mzazi akiwa msimamizi wa kila hatua ya maendeleo ya mtoto," alieleza Yusuph Kuonewa.
Wananchi hao walihitimisha kwa kutoa wito kwa serikali, mashirika ya kiraia, na viongozi wa dini na jamii kushirikiana kwa karibu katika kutoa elimu kuhusu haki za mtoto, na kuhakikisha sheria za kulinda watoto dhidi ya ajira haramu na unyanyasaji zinasimamiwa ipasavyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED