Vyama vya Msingi vya Ushirika vyatakiwa kuwa na mipango endelevu ya maendeleo
By
Stevie Chindiye
,
Nipashe
Published at 01:00 PM Apr 29 2025
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Muungano wa Vyama Vikuu vya Ushirika wa Wakulima wa Korosho Kanda ya Kusini, Odas Mpunga.
Mwenyekiti wa Muungano wa Vyama Vikuu vya Ushirika wa Wakulima wa Korosho Kanda ya Kusini, Odas Mpunga, amevitaka vyama vya msingi (AMCOS) kuwa na mipango dhabiti ya kuanzisha miradi ya maendeleo ili kuachana na utegemezi wa ushuru kama chanzo kikuu cha mapato.
Mpunga alitoa wito huo wakati akizungumza na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 22 wa kawaida, uliofanyika katika ukumbi wa Sky Way mjini hapa.
Akifafanua zaidi, Mpunga alisema kuwa bila AMCOS kuwa na mipango endelevu ya maendeleo, itakuwa vigumu kwa vyama hivyo kupiga hatua za maendeleo kwa kutegemea ushuru pekee.
"Bila kuwa na mikakati ya maendeleo ya muda mrefu, AMCOS zitaendelea kusuasua. Tunahitaji mipango inayolenga kubuni vyanzo mbadala vya mapato," alisema.
Alieleza kuwa tayari Vyama Vikuu vyote vinavyohusishwa na zao la korosho katika kanda hiyo, ambavyo ni MAMCU, RUNALI, TAMCU, na TANECU, vimeanza kuchukua hatua kwa kununua mali mbalimbali pamoja na kuwekeza katika miradi ya viwanda na hoteli kama sehemu ya juhudi za kupunguza utegemezi wa ushuru.
Katika hotuba yake, Mpunga pia aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa viuatilifu na pembejeo za ruzuku kwa miaka mitatu mfululizo, hali iliyosaidia kupunguza gharama kwa wakulima wa korosho.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Abdalah Mtila, aliipongeza TAMCU kwa usimamizi mzuri wa ugawaji wa pembejeo kwa wakulima wa korosho.
"Utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi na usimamizi wa viongozi wa TAMCU katika ugawaji wa pembejeo umepunguza kero kwa wananchi, ambao wengi wao ni wakulima wa zao hili," alisema Mtila. 1