USHIRIKA wa Wanafunzi wa Kikristo Tanzania (TAFES), unahitaji kukusanya kiasi cha shilingi milioni 450 katika kampeni ya kufanikisha ukarabati na uboreshaji wa Kituo cha Uwezeshaji na Ustawi wa Jamii, kilichopo Boko, Dar es salaam .
Kuelekea maadhimisho ya kitaifa ya miaka 35 ya TAFES yatakayofanyika Juni 14, mwaka huu, kiongozi wa wahitimu na mwakilishi kutoka OPM wa TAFES Dk. Charles Sokile, amesema kituo hicho kitakuwa kinatoa huduma mbalimbali kwa wanafunzi zaidi ya 6000.
Amesema kuwa kuwezesha Tafes kutapanua huduma zake, ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi vyuoni na hivyo kutoa usaidizi kamili, kwa wanafunzi wanaokabiliwa na changamoto za kitaaluma, kihisia na kijamii.
"Kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 35 ya TAFES tuna wakaribisha wadau wote wenye mapenzi mema na ustawi wa vijana na jamii kwa ujumla kuungana nasi katika kampeni ya kukusanya fedha hizi," amesema Dk. Sokile.
Amebainisha mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 35 ya huduma ni pamoja na kutengeneza viongozi wenye maadili na uraia mwema 2000, kutoa fursa kwa wahitimu kujitolea kwa lengo la kuongeza uzoefu, kuanzisha kampeni mbalimbali, kwa ajili ya kuelimisha vijana.
Ameeleza mafanikio mengine ni kuwafikia wahitaji kwenye jamii, kuendesha makongamano kipindi cha pasaka na krisimasi kwa wanafunzi zaidi ya 2000, kwa mikoa tisa kila mwaka kuanzisha makundi ya wanataaluma zaidi ya 10.
"Mpaka sasa, juhudi zetu katika kuboresha maisha ya vijana walioko vyuo vikuu na vyuo vya kati zimeenea katika mikoa 18 nchini, tukishirikiana na vyuo vikuu vya kati zaidi zaidi ya 90, washirika hai 1,090, taasisi na kampuni zaidi ya 12," ameongeza.
Makamu Mwenyekiti wa wahitimu, Rodney Alananga, amewataka wahitimu wenzake kutumia mbinu walizozipata kwa kuwasaidia vijana ambao hawajasoma, ili kuwasaidia changamoto zao.
"Ninaomba wahitimu wenzangu watumie vizuri mbinu walizozipata kwa kuwawezesha vijana mara nyingi tumekuwa tukikutana na vijana wengi wenye uwezo wa kufanya kazi isipokuwa wanashindwa kutimiza malengo, kwa sababu hawana wa kuwawezesha, amesema Alanga.
Airis Dions, ambaye ni mwanafunzi anayesomea shahada ya ufamasia amewataka wanafunzi wenzake wajitoe kuchangia fedha hizo, ili waweze kukamilisha malengo yao.
"Ni wakati wa wanafunzi wenzangu kila mmoja kwa wakati wake kuchangia fedha hizi kwani taasisi hii inawasaidia vijana.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED