Serikali ya Tanzania imetangaza kuchukua hatua kali dhidi ya Malawi na Afrika Kusini kufuatia vikwazo vya kibiashara vinavyowakwamisha wakulima na wafanyabiashara wa Kitanzania kuuza bidhaa zao katika nchi hizo.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema Malawi imezuia kuingiza bidhaa kama mchele, unga, ndizi, mahindi na tangawizi kutoka Tanzania, hali iliyowaathiri wafanyabiashara wengi. Vilevile, Afrika Kusini imeendelea kufunga soko la ndizi kwa Tanzania licha ya juhudi za muda mrefu za kidiplomasia.
📌Kuzuia uingizwaji wa bidhaa zote za kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini hadi masoko yao yatakapofunguliwa kwa bidhaa za Tanzania.
📌Kuzuia bidhaa kutoka nchi hizo kupitishwa ndani ya Tanzania au kutumia Bandari ya Dar es Salaam kuelekea nchi nyingine.
📌Kusitisha usafirishaji wa mbolea kwenda Malawi kama njia ya kulinda maslahi ya wakulima wa Tanzania.
Waziri Bashe amesema juhudi za mawasiliano na Malawi hazijazaa matunda, na hatua hizo ni kulinda uchumi wa taifa, heshima ya wakulima na kudai usawa wa kibiashara katika ukanda wa SADC.
Ameonya wafanyabiashara waache mara moja kuagiza bidhaa kutoka Afrika Kusini, ikiwemo tufaa (apples) na machungwa, hadi pale nchi hiyo itakapofungua soko la ndizi kwa Tanzania.
Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kuchukua hatua zaidi endapo hali haitabadilika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED