WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, amewataka wazazi na walezi kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto kutokana na utafiti kuonesha ndugu na jamaa wa karibu ndio wanaongoza kuwafanyia ukatili.
Dk. Gwajima, alibainisha hayo juzi kwenye taarifa yake iliyotolewa kwa umma kulaani tukio la mauaji ya mtoto Grayson Kanyenye (6), anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa na kitu kizito katika eneo la Ilazo, jijini hapa.
Mtoto huyo anadaiwa kuuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani wakati mama yake akiwa ametoka kwenda kutembea usiku wa kuamkia Sikukuu ya Krismasi na kumwacha kwa dereva wa bodaboda.
Katika taarifa yake Dk. Gwajima alisema wizara imepokea taarifa hizo za masikitiko kwa simanzi kubwa kutokana na mtoto huyo kukatishwa uhai wakati alikua anaanza safari ya ndoto yake.
“Natoa pole nyingi kwa wazazi wa mtoto ndugu na jamaa kwa msiba huu mkubwa uliogusa hisia za wengi, natoa wito kwa wazazi na walezi kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto na kukumbuka kuwa tafiti zinaonesha ndugu na jamaa wa karibu ndiyo wanaongoza kuwafanyia watoto ukatili ikiwa ni pamoja na ubakaji, ulawiti na hata mauaji,” alisema Dk. Gwajima.
Aidha, alisema ni imani yake kuwa vyombo vya kusimamia sheria vitafuatilia jambo hilo kwa kadri iwezekanavyo ili wahusika wabainike na haki ya mtoto ipatikane na kuwa funzo kwa wengine wanaofanya ukatili.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi, akizungumzia tukio hilo juzi, alisema mwili wa mtoto huyo ulikutwa ndani ya nyumba ukiwa na majeraha shingoni.
Katabazi, alisema tukio litokea majira ya saa 1:00 asubuhi katika Mtaa wa Bwawani, Ilazo Extension jijini Dodoma, nyumbani kwa Ofisa Uvuvi wa Mtera, Hamis Mohamed.
Alisema, Hamis na mama wa mtoto huyo walitoka kwenda matembezini na kumwacha chini ya usimamizi wa dereva bodaboda maeneo ya Ilazo Extension jijini hapa, Kelvin Gilbert.
Alisema, inadaiwa kuwa bodaboda huyo walimfahamu kupitia huduma ya usafiri anayoitoa kwa familia hiyo.
“Bodaboda huyu aliachiwa mtoto ili amwangalie kipindi ambacho watakuwa kwenye matembezi wawili hao wakati wa usiku, lakini waliporudi mtoto hawakumuona hadi asubuhi majira ya saa 1:00 walipomkuta kwenye chumba akiwa ameuawa na alama za kupigwa na kitu kizito shingoni mwake,” alisema.
Kadhalika, Kamanda Katabazi alisema Jeshi la Polisi mkoani hapa linamshikilia bodaboda huyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa tukio hilo la mauaji.
“Tumemkamata bodaboda huyo kwa ajili ya uchunguzi wa tukio hili ambapo yeye amekanusha kuhusika na jambo hili, lakini tunaendelea na uchunguzi ili kubaini nini hasa kilitokea kwa mtoto huyu na kupelekea kifo chake,” alisema Katabazi.
Aidha, Kamanda alitoa wito kwa wazazi kuacha tabia ya kukabidhi watoto wao kwa watu ambao hawawajui vizuri ili kuepusha matukio kama hayo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED