Jela miaka 3 kwa udanganyifu mitihani ya taifa

By Jaliwason Jasson , Nipashe
Published at 02:34 PM Jun 26 2024
MAHAKAMA ya Wilaya ya Babati, mkoani Manyara.
Picha: Maktaba
MAHAKAMA ya Wilaya ya Babati, mkoani Manyara.

MAHAKAMA ya Wilaya ya Babati, mkoani Manyara, imewahukumu watu wawili kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela kila mmoja, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kufanya udanganyifu wa kuwafanyia mitihani ya taifa wanafunzi wa kidato cha nne na kughushi nyaraka.

Waliohukumiwa adhabu hiyo, ni Jacob Dezderi (21), Mkazi wa Bashneti, Wilaya ya Babati na Paschal Sikai (33), Mkazi wa Dareda, ambaye alikuwa Mwalimu wa kujitolea.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Victor Kimario, alisema mahakama hiyo imejiridhisha kwamba washtakiwa hao walifanya udanganyifu huo mwaka 2023, kwa kuwafanyia mitihani wanafunzi wa kujitegemea, kisha kughushi nyaraka za barua ya utambulisho wa kufanyia mitihani.

Kwa mujibu wa hakimu Kimario, makosa hayo waliyafanya Novemba 13 na 14 mwaka jana.

Alisema washtakiwa walikamatwa Novemba 14 mwaka 2023, baada ya kukiuka Sheria ya Baraza la Mitihani la Tanzania, Kifungu cha 19 (a) na Kifungu 24 (1), Sura 107 iliyofanyiwa Marejeo Mwaka 2019.

Washtakiwa hao kwa pamoja walikiuka matakwa ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Kifungu cha 333,  335 (a) na 337, Sura ya 16, iliyofanyiwa Marejeo ya Mwaka 2022.

Aidha, Hakimu Kimario, alisema mshtakiwa namba moja, alijifanya kuwa anaitwa Daudi Buxay, na mshtakiwa  wa pili, alijiita Isaya Mtinda na wote walikuwa wakiwafanyia mitihani watahiniwa wa kujitegemea katika Shule ya Sekondari Endamanang,' na walinaswa wakiwa kwenye mtihani wa Hisabati huku wakiwa tayari walishafanya mitihani ya Uraia na Kingereza.

Alisema mahakama ilipomhoji mshtakiwa namba moja, Jacob Dezderi, alidai kuwa aliitwa kutoka Mbeya, kwa ajili ya kazi maalum, ila hakuithibitishia mahakama ni kazi gani, huku mshtakiwa wa pili, akikana mbele ya mahakama kuwa hakuwapo.

Akisoma hukumu hiyo, hakimu Kimario alisema kitendo walichokifanya siyo hasara kwao au kwa wateja wao bali ni hasara kwa taifa na jamii kwa ujumla, kwa kusababisha madhara ambayo pengine yanaweza kuligharimu taifa kwamba kama ni daktari anaweza kudunga mgonjwa sindano kumbe hakustahili.

Awali, Wakili wa Serikali, Leonce Bizimana, alidai mahakamani hapo kwamba kosa walilolifanya la udanganyifu wa kuwafanyia mitihani watu wengine, lina athari hasi  katika taifa.