HESLB yatangaza msako wa wadaiwa sugu mikopo yake

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 10:42 AM Jun 29 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imezindua kampeni maalum ya kusaka wadaiwa sugu 50,000 ambao ni wanufaika wa mikopo ili kukusanya Sh. bilioni 200.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia, alisema kampeni hiyo waliyoipa jina la 'FICHUA KUWA HERO WA MADOGO', ilianza rasmi jana.

Dk. Kiwia alisema lengo la kampeni hiyo ni kuhamasisha Watanzania kushirikiana na HESLB kufichua wadaiwa sugu walioko ofisini, nyumbani, mitaani na kwingineko, ili fedha hizo zikusanywe na kusaidia wengine wenye uhitaji.

Alisema kampeni hiyo itasaidia na kuchochea zaidi kuongeza uwezo wa kutoa mikopo na kuongeza kiwango cha mikopo.

Dk. Kiwia alisema wadaiwa hao watawapata kwa kutumia wanafunzi, watu mashuhuri, mitandao ya kijamii, vyombo vya habari, kampuni simu na wananchi wazalendo ambao wana uchungu na maendeleo ya elimu nchini.

"Lengo ni kufichua wadaiwa sugu ambao wana vipato, lakini wako mitaani wanaendelea na shughuli zao na hawashtuki kulipa madeni.

"Tunashukuru kuna baadhi ya wananchi wazalendo walikuwa wakitutumia majina ya watu wao wa karibu na tunawafuatilia, alisema Dk. Kiwia.

Akizungumzia hali ya urejeshaji mikopo, Mkurugenzi wa Urejeshaji na Urejeshwaji Mikopo HESLB, George Mziray, alisema ni nzuri na wamekuwa wakikusanya wastani wa Sh. bilioni 15 kwa mwezi kutoka kwa wanufaika 220,000 ambao wameajiriwa na kujiajiri.

Alisema endapo watawafikia wadaiwa wote, kiasi cha fedha kitakachokusanywa kitakuwa ni Sh. bilioni 200.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema bungeni jijini Dodoma jana kuwa HESLB imeendelea kukusanya mikopo iliyoiva kutoka kwa wanufaika wa mikopo.

"Kwa mwaka 2023/24, serikali ilipanga kukusanya Sh. bilioni 230 ambapo hadi kufikia Mei 2024, Sh. bilioni 161 zilikusanywa sawa na asilimia 70 ya lengo," alisema.

Majaliwa pia alisema kuwa kwa mwaka 2024/25, serikali imetenga Sh. bilioni 787 kwa ajili ya kukopesha wanafunzi 250,000, wakiwamo 80,000 wa shahada ya kwanza ambao ni wapya.

"Maandalizi ya awali yameanza ikiwa ni pamoja na kusambaza mwongozo wa upangaji na utoaji mikopo; kufungua dirisha la uombaji mikopo kwa mwaka 2024/25 kwa muda wa siku 90 kuanzia Juni Mosi hadi 31 Agosti 2024;  na kutoa elimu kwa waombaji mkopo na wadau wengine," alisema.

Majaliwa alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/24, serikali ilitoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu 224,056 na hadi kufikia Juni mwaka huu, wanafunzi hao walikuwa wamepatiwa mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 743.2 sawa na asilimia 94.6 ya fedha zilizotengwa.

Mikopo hiyo ilitengwa kwa ajili ya wanafunzi wa ngazi ya stashahada, shahada ya awali, stashahada ya juu ya mafunzo ya sheria kwa vitendo, shahada za umahiri na uzamivu, na ufadhili wa Samia (Samia Scholarships) katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.

Wanafunzi mnufaika Khadija Sultani anayesomea Shahada ya Usimamizi wa Biashara katika Chuo cha Kikuu cha Tumaini na Japhet Makyao anayechukua Shahada ya Udaktari na Upasuaji katika Chuo Kikuu cha Kimataifa Kampala, wameomba Watanzania kurejesha mikopo hiyo ili wenzao wengine wanufaike.

Wawili hao walisema jana katika ofisi za HESLB jijini Dar es Salaam kwamba kupitia bodi hiyo wameweza kutimiza ndoto zao kielimu kwa kuwa wasingemudu gharama kutokana na kufiwa na wazazi wao.