Nyanduga: Sera ya Uhifadhi inawajali zaidi wanyamapori

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 08:48 AM Jun 29 2024
Mwenyekiti mstaafu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Wakili Mwandamizi Bahame Nyanduga.
Picha: Maktaba
Mwenyekiti mstaafu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Wakili Mwandamizi Bahame Nyanduga.

KITENDO cha Sera ya Uhifadhi kumpa kipaumbele mnyama kuliko binadamu kimetajwa kuwa ni moja ya sababu za uvunjifu wa haki za binadamu hususani kwa wanaopakana na hifadhi za taifa.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti mstaafu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Wakili Mwandamizi Bahame Nyanduga wakati wa uzinduzi wa ripoti ya masuala ya uhifadhi na haki za binadamu.

Ripoti hiyo ni matokeo ya utafiti na uchunguzi uliofanyika nchi nzima kuhusiana na madhila ya mara kwa mara yanayowafika wanaoishi karibu na hifadhi za taifa na kushauri hatua za kuchukua.

Wakili Nyanduga alisema kwa kushirikiana na wadau wengine, wameamua kufanya utafiti huo kutokana na kuwapo malalamiko ya ukiukwaji haki za binadamu kwa wanaoishi jirani na hifadhi.

Alisema lengo lao, pamoja na mambo mengine, ni kuonesha namna haki za binadamu zinavyokiukwa na Jeshi la Polisi pale serikali inapotekeleza masuala ya uhifadhi. 

"Ninakubali na ninatambua umuhimu wa hifadhi, lakini ninapendekeza uhifadhi endelevu. Ukiangalia sera na taratibu, nyingi zimewalenga wanyamapori au misitu na kusahau binadamu.

"Kuna haja kuelimisha wananchi kuhusu hifadhi, kuzingatia sheria hasa pale panapokuwa na mjadala katika kuelewa sheria ili pasiwe na marudio ya hizi changamoto za mara kwa mara," alishauri Wakili Nyanduga.

Ofisa Mtendaji Mkuu Brain Media, Jesse Kwayu, alisema jamii zinazoishi karibu na hifadhi zinakumbwa na madhara mengi, ikiwamo kuteswa, kupigwa, kuuliwa na kunyang'anywa mali zao. 

Alisema matukio mengine katika ripoti hiyo yanatisha, akigusia kuwa zipo simulizi za waliopoteza ndugu zao na kuporwa mali zao.

Kwayu alisema kuna haja kuwa na mkutano wa kitaifa wa kujadili masuala hayo ya uhifadhi na haki za binadamu.

Akisimulia namna alivyopata madhara kwa kuishi jirani na hifadhi katika Kijiji cha Ulukugwado, mkoani Arusha, Angelina Nassari alisema: 

"Mwaka 2017, kijijini kwetu walikuja watu wa  hifadhi na Jeshi la Polisi, walitufuata na kutuuliza 'kwanini mnaishi hifadhini?' Walikuwa wengi wakaanza kuturushia mabomu ya moshi na kututimua. 

"Walirudi tena katika eneo tunalootesha mazao, wakasema ndani ya saa 24 hawataki kuona mtu katika eneo tunamoishi, wakapiga mabomu, wakaua mbuzi na ng'ombe wangu.

"Kule nilikotokea tunateseka sana, tunaishi kama bundi, hakuna taarifa wala ushirikishwaji wowote, ukiuliza wanakwambia ni uamuzi kutoka ngazi za juu, maana kule tunaishi kama wakimbizi."

Angelina aliomba serikali iangalie namna ya kuwasaidia ili waishi kwa amani kama ilivyo kwa raia wengine wasiopakana na hifadhi.

Mwathirika mwingine anayeishi jirani na Pori la Akiba Selou mkoani Lindi, Kasimu Mkwanga, alisema wakazi wa eneo hilo wanaishi kwa hofu kwa kile alichodai kipande walichopewa waishi kwa muda baada ya kuhamishwa kinguvu kutoka eneo hilo walikokuwa, nacho kuna mwekezaji mwindaji anakitaka.

"Jambo hili linatuacha njiapanda, hatujui nini cha kufanya, tukikumbuka tulipokuwa tunaishi mwanzo, tulihamishwa kwa kupigwa na mabomu ya moshi na risasi pia, walivunja nyumba zetu na hatujalipwa chochote tangu siku hiyo mpaka leo (jana)," alisimulia.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2021/22, ina taarifa kuhusu madhila ya watu wanaoishi karibu na hifadhi, ikijumuisha matukio ya kuuliwa na kujeruhiwa na wanyamapori.