KUCHELEWA KULIPA MAFAO: 'Waajiri wanaokiuka wajibu wao washitakiwe'

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 08:52 AM Jun 29 2024
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka mifuko ya hifadhi ya jamii kuchukua hatua dhidi ya waajiri wote wanaokiuka kwa makusudi wajibu wao wa kuwasilisha michango ya wanachama kwa wakati.

Majaliwa alitoa agizo hilo jana bungeni jijini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 15 Bunge. Bunge limeahirishwa hadi Agosti 27 mwaka huu.

"Bodi na menejimenti za mifuko tumieni vifungu vya sheria katika kuhakikisha michango inawasilishwa kwa wakati ili kuwaondelea wastaafu changamoto za kulipwa mafao kwa kuchelewa," aliagiza Majaliwa.

Waziri Mkuu alisema kuwa katika kuhakikisha wastaafu wanalipwa kwa wakati, sheria za mifuko zinaelekeza mwajiri kuwasilisha taarifa ya maandishi katika mfuko ndani ya miezi sita kabla ya mtumishi kustaafu, ili mfuko uweze kuanza taratibu za kuandaa mafao ya mwanachama.

Alisema mifuko nayo inatakiwa ndani ya siku 60 baada ya mwanachama kustaafu iwe imeshamlipa mafao yake kama madai yake yatakuwa hayana kasoro na michango imewasilishwa kwa ukamilifu.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2023/24, asilimia 90 ya madai ya wastaafu yamelipwa ndani ya muda wa siku 60 kwa mfuko wa NSSF na asilimia 61 kwa mfuko wa PSSSF.

"Sababu za baadhi ya wastaafu kutolipwa kwa wakati ni pamoja na michango yao kucheleweshwa kuwasilishwa katika mifuko na baadhi ya wastaafu kubadilisha kumbukumbu za utumishi kama vile tarehe ya kuzaliwa, majina na muda wa kuanza kazi," alisema.

Majaliwa alisema ili kukabiliana na tatizo la ucheleweshaji michango kutoka kwa waajiri, serikali imewasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria za Mifuko unaolenga kuzipa nguvu Bodi za Wadhamini za Mifuko kupunguza au kusamehe kabisa tozo zinazotokana na ucheleweshaji michango.

Alisema marekebisho hayo yatawezesha waajiri wenye malimbikizo makubwa ya michango kulipa madeni yao na kuhakikisha wastaafu wanalipwa kwa wakati baada ya kulitumikia taifa lao.

"Nitoe rai kwa waajiri wote kuhakikisha wanalipa michango ya watumishi wao kwa wakati na kuondoa usumbufu wa kucheleweshwa kulipwa kwa watumishi hao pindi wanapostaafu.

"Niitake pia mifuko kuchukua hatua kwa waajiri wanaokiuka kwa makusudi wajibu wao wa kuwasilisha michango kwa wakati," Waziri Mkuu aliagiza.

Majaliwa pia alisema serikali inaboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kwa kutekeleza afua mbalimbali za kikodi na kiutendaji.

Hata hivyo, alisema kumekuwa na changamoto ambazo zimeendelea kujitokeza na kusababisha taharuki na sintofahamu nyingi hasa kwa wafanyabiashara nchini.

"Sintofahamu hizo kama ambavyo waheshimiwa wabunge walivyochangia humu bungeni katika siku za hivi karibuni ni pamoja na migomo ya wafanyabiashara wetu kutoka katika maeneo tofauti tofauti nchini," alisema.

Majaliwa alisema sehemu kubwa ya madai ya wafanyabiashara inatokana na hoja takribani 41 ambazo ziliwasilishwa na viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT).

Alisema kati ya hizo, hoja sita zilikuwa za kisera na kisheria na zilizobaki 35 ni za kiutendaji ambapo serikali imefikia mwafaka katika kutatua kero zao.

"Serikali kwa pamoja na uongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini tumeafikiana kusimamia maazimio kama yalivyowasilishwa na Msemaji Mkuu wa Serikali.

"Nitumie fursa hii mbele ya Bunge lako Tukufu kuziagiza mamlaka zote za serikali kuhakikisha maazimio yote yanatekelezwa kwa ufasaha na kwa wakati uliokubalika na pande zote (yaani muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu)," alisema.

Waziri Mkuu pia alisema serikali imekamilisha maandalizi ya uratibu wa upelekaji fedha za mikopo ya asilimia 10 katika mamlaka za serikali za mitaa kwenda mfuko wa mikopo ya vikundi na kusimamia urejeshwaji wa mikopo iliyotolewa miaka ya nyuma.

"Itakumbukwa kwamba mwezi Aprili 2023, serikali ilisitisha utoaji mikopo hii kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

"Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa fedha 2023/24, serikali imekamilisha maandalizi ya uratibu wa upelekaji fedha hizo katika mamlaka za serikali za mitaa kwenda kwenye mfuko wa mikopo ya vikundi na kusimamia urejeshwaji mikopo iliyotolewa miaka ya nyuma," alisema.

Alisema katika mwaka wa fedha 2024/25, serikali imepanga kutoa mikopo ya Sh. bilioni 228 ambapo kati ya hizo, Sh. bilioni 63.7 ni fedha za marejesho zilizokuwa zikiendelea kukusanywa kutokana na mikopo iliyotolewa kabla ya kusimamishwa Aprili mwaka jana.

Alisema Sh. bilioni 63.2 ni fedha zilizokuwa zinatengwa kwa ajili ya mikopo na Sh. bilioni 101.1 ni fedha ambazo zimetengwa kutokana na makisio ya makusanyo ya mapato ya ndani ya mwaka 2024/25.

Majaliwa alisema serikali imepanga utaratibu wa kutumia benki kwa halmashauri 10 za majaribio ambazo ni Majiji ya Dar es Salaam na Dodoma, Manispaa za Kigoma Ujiji na Songea, Miji ya Newala na Mbulu, Wilaya za Siha, Nkasi, Itilima na Bumbuli.