Kariakoo yote sasa kufungwa kamera

By Restuta James , Nipashe
Published at 09:30 AM Dec 04 2024
news
Picha: Mtandao
Kamera.

SASA ni rasmi serikali inakusudia kufunga kamera za ulinzi (CCTV), katika eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, ili kudhibiti uhalifu na kuwezesha biashara kufanyika kwa saa 24.

Mkurugenzi wa Jiji la Ilala, juzi alitoa taarifa ya kumtafuta mzabuni akayetekeleza kazi hiyo na jana ilikuwa ni siku ya kutembelea eneo kamera zitakapofungwa, kuanzia Polisi Msimbazi.

Katika taarifa hiyo, mkurugenzi huyo alisema kazi hiyo inaweza kufanywa na kampuni binafsi, taasisi au ubia.

“Tangazo la usambazaji na ufungaji wa kamera za CCTV Kariakoo awamu ya kwanza…kampuni za serikali, za ndani, za kigeni, kikundi maalumu, mtengenezaji wa ndani, ubia, mtengenezaji wa nje ya nchi, ushirikiano wa kampuni za ndani na nje, wanaitwa kushiriki,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Ilieleza kuwa fedha za kufunga kamera hizo zimetengwa na serikali katika bajeti yake ya mwaka huu wa fedha, 2024/2025.

“Serikali imetenga fedha kwa ajili ya uendeshaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025. Inakusudiwa kuwa sehemu ya mapato ya mfuko itatumika kulipia malipo stahiki chini ya mkataba wa ufungaji wa kamera ya CCTV awamu ya kwanza katika eneo la Kariakoo,” ilifafanua.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii jana, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, alisema Kariakoo itafungwa kamera na taa, ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, kutaka biashara katika eneo hilo zifanyike kwa saa 24.

“Tunafunga kamera na taa kwa pamoja. Lengo ni kuimarisha ulinzi na pia kuwezesha biashara zifanyike kwa saa 24,” alisema.

Akiwa katika ziara ya kikazi mwezi uliopita, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema serikali inakusudia kufunga kamera hizo katika maeneo mbalimbali ya jiji ili kuimarisha ulinzi.

Alisema kamera na taa zitafungwa kwenye maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu ikiwamo Kariakoo.

Serikali inakusudia kufunga taa na kamera za ulinzi, wakati ambao Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameunda Kamati ya Wataalamu ya Uchunguzi wa majengo katika eneo la Kariakoo.

Kamati hiyo iliundwa baada ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa tatu katika eneo la Kariakoo na kusababisha vifo vya watu 31 na wengine 88, kujeruhiwa Novemba 16, mwaka huu.

Aliiagiza itekeleze majukumu yake kwa kufuata sheria, kanuni na maadili ya kazi, kwa kuchunguza uimara wa majengo yanayojengwa, kuchunguza endapo taratibu zinafuatwa wakati wa ujenzi, ikiwamo vibali, makandarasi wenye sifa na usimamizi wa mamlaka husika wakati wa ujenzi.

Waziri Mkuu alisema madhumuni mengine ya kuundwa kwa kamati hiyo ni pamoja na kuchunguza endapo uboreshaji majengo unaofanywa Kariakoo unazingatia sheria, kanuni na taratibu pamoja na kubainisha majengo yote yaliyo katika hatari ya kuanguka na kupendekeza hatua za kuchukua.

Aidha, zinafungwa wakati ukarabati wa soko la Kariakoo ukiwa umefikia asilimia 90 na kugharimu Sh. bilioni 28.

Akiwa mkoani Kagera, Agosti mwaka huu, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, alisema serikali iko mbioni kufunga kamera za uchunguzi 6,500 kwa kuanzia na majiji makuu manne, ili kupunguza uharibifu na kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi.

Alisema kamera zitafungwa katika maeneo ya mikusanyiko ya watu kama vile maeneo ya masoko, viwandani na kwenye kampuni katika majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Dodoma.

Aidha, kamera hizo zitafungwa chini ya mradi wa Jeshi la Polisi wa majiji salama na kwamba bajeti ya utekelezaji imetengwa katika mwaka huu wa fedha 2024/25.