Miili sita yatambuliwa ajali ya Kibaoni

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 01:34 PM Dec 28 2024
Miili sita yatambuliwa ajali ya Kibaoni
Picha:Mtandao
Miili sita yatambuliwa ajali ya Kibaoni

WAKATI idadi ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea Kijiji cha Kibaoni-Tarakea, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro ikifikia 10, hadi sasa waliotambuliwa ni watu sita pekee.

Ajali hiyo iliyotokea barabara kuu ya Moshi/Tarakea, majira ya saa 9:40 jioni ya Desemba 26, mwaka huu, ilihusisha basi la abiria, mali ya Kampuni ya Ngasere, lenye namba za usajili T 620 DZQ lililokuwa likitokea Dodoma kwenda Tarakea, kugongana uso kwa uso na gari dogo la abiria aina ya Toyota Noah, namba T 959 CKU, lililokuwa lilitokea Tarakea kwenda Moshi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani humo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Simon Maigwa, mpaka sasa waliotambuliwa ni watu sita kati ya 10 waliokuwamo ndani ya Noah.

Aliwataja waliotambuliwa kuwa ni Mamasita Lowassa (27), mkazi wa Kamwanga ambaye alikuwa dereva wa Noah na Damarisi Mwikau (22), mkazi wa Elast, nchini Kenya.

Wengine ni Peter Urio (38), Monica Mumbua, raia wa Kenya, Eligatanasi Kanje (30), mkazi wa Tarakea na Hilda Liberatus (24), mkazi wa Kikelelwa, huku polisi ikieleza miili ambayo bado haijatambuliwa ni minne.

Aidha, Kamanda Maigwa ametaja chanzo cha ajali hiyo, ni uzembe wa dereva wa gari dogo la abiria aina ya Noah kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari.

Jana katika ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Rais Samia Suluhu Hassan alisema:

"Nimesikitishwa na taarifa ya vifo vya ndugu zetu tisa kutokana na ajali ya barabarani iliyotokea katika barabara ya kutoka Tarekea, Wilaya ya Rombo kuelekea mji wa Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro. 

"Ninawaombea marehemu wapumzike kwa amani. Ninatoa salamu za pole kwa wafiwa, ndugu na jamaa na ninawaombea majeruhi wapate nafuu kwa haraka.

...Nasisitiza madereva kuendelea kuwa makini na waangalifu zaidi barabarani, huku Jeshi la Polisi likiendelea na kazi ya kusimamia sheria za usalama barabarani wakati huu wa mwisho wa mwaka."