Naibu Waziri awatuhumu rushwa watumishi TBS, WMA

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 11:56 AM Feb 21 2025
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe.

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, amesema baadhi ya watumishi wa Wakala wa Vipimo (WMA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wamekuwa wanapokea rushwa na kuruhusu bidhaa duni na kuendelea kuuzwa mitaani, hivyo kuhatarisha afya za watumiaji.

Kigahe alisema hayo jana wakati akizungumza na watumishi baada ya kutembelea na kupewa taarifa ya Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na WMA mkoa wa Singida kuhusu utendaji kazi katika siku ya tatu ya ziara yake mkoani hapa.

"Maelekezo ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo, ni kwamba  ingieni mitaani kusaka bidhaa. Kama  zinazalishwa mwende kwa wenye viwanda muwasaidie wazingatie sheria za nchi. Wale  ambao hawatazingatia maelekezo ya serikali hatua zichukuliwe," alisema.

Kigahe alisema pia kuna viwanda bubu vingi ambavyo vimeanzishwa na vinazalisha bidhaa ambazo hazina ubora, hivyo kunahitajika kufanya uchunguzi wa kina kuvitafuta viliko na kuchukua hatua dhidi ya wamiliki.

"Unakuta raia wa kigeni anakodi nyumba lakini huko nyuma anazalisha bidhaa au anakodi godauni na kuingiza bidhaa kutoka nje ambazo hazina ubora halafu anatafuta vijana wamachinga wanaziuza kwa bei nafuu. Yaani wanakuwa hawana maduka rasmi wala leseni na hawalipi kodi ya serikali," alisema.

Naibu Waziri alisema lengo la serikali ni kuhakikisha  viwanda vya ndani vinalindwa ili vizalishe bidhaa bora zenye ushindani kwenye soko ndani na la nje na kuzitaka TBS na WMA kutoa elimu kwa wazalishaji kuhusu ubora wa bidhaa wanazozalisha.

"Bidhaa ambazo zinazalishwa na baadhi ya viwanda ambavyo wakati mwingine havijulikani vimeingiliwa na hawa wageni lakini na wengine ni Watanzania na wanazalisha maeneo ambayo hayatambuliki na hazina nembo inayoonesha zimezalishwa wapi, " alisema.

Kigahe alisema kwa sheria za Tanzania, mteja anayenunua bidhaa hajajua na akikamatwa njiani anayepaswa kuchukuliwa hatua ni mzalishaji kwanza na baadaye mteja aliyenunua.

Naibu Waziri alizitaka taasisi zinazohusika na kupima na kuangalia ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini, zisiwe zinakimbilia kuvifunga viwanda au wajasiriamali wanaozalisha bidhaa badala yake ziwasaidie kwanza kwa kuwapa elimu ili kuzalisha bidhaa bora.

"Tuwasaidie wajasiriamali badala ya kumdhibiti kwa kumfungia kiwanda. Tumsaidie  kwanza kumwelimisha. Kumfungia  si sifa maana mtu anakuwa amewekeza fedha zake," alisema.