Rais Mwinyi akubali kutekeleza maombi ya Makonda

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 08:25 PM May 17 2024

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kutekeleza maombi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda, katika suala la uwekezaji wa ujenzi wa hoteli na nyumba za kulala wageni.

Mwinyi aliyasema hayo leo baada ya kupokea maombi kutoka kwa Makonda  kwenye semina maalum ya wanahisa wa benki ya CRDB iliyofanyika Kituo cha Mikutano Cha Kimataifa Arusha (AICC).

Amesema kutokana na idadi kubwa ya wawekezaji wanaofika Zanzibar kutaka kuwekeza kwenye ujenzi wa nyumba na vyumba vya kulala wageni na watalii wanaofika nchini watafanyia kazi ombi hilo.

Awali mMakonda amemuomba Rais Mwinyi kuiunganisha Zanzibar na Mkoa wa Arusha kwenye sekta ya utalii ili kuwezesha mabadilishano ya watalii.
 
Aidha, amemuomba Rais Mwinyi kutangaza fursa na vivutio vya uwekezaji vilivyo mkoani Arusha kwa lengo la kutimiza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, ya kuongeza vyumba na vitanda vya kulala wageni mkoani Arusha.

Makonda ameishukuru benki ya CRDB kwa kuwa mdau mkubwa wa maendeleo ya Mkoa wa Arusha na kuichagua Arusha kuwa mwenyeji wa semina ya wanahisa na Mkutano Mkuu wa 29 wa wanahisa unaotarajiwa kufanyika Mei 18, 2024 Jijini Arusha.