Ridhiwani awapa neno vijana waokwenda Ulaya kikazi

By Restuta James , Nipashe
Published at 05:39 PM Dec 03 2024
Ridhiwani awapa neno vijana waokwenda Ulaya kikazi.
Picha: Restuta James
Ridhiwani awapa neno vijana waokwenda Ulaya kikazi.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, amewafunda vijana 26 waliopata fursa ya kwenda kwenye mafunzo ya vitendo nje ya nchi, akiwataka wawe mabalozi wa Tanzania, kwa kufanyakazi kwa bidii.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Ushirika cha Wajasiriamali Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUGECO), Revocatus Kimario, amewapa changamoto wanafunzi waliopo vyuoni, kutumia muda wa ziada kujiendeleza katika lugha za kimataifa, ili kufungua milango ya kufanyakazi nje ya nchi.

Waziri Ridhiwani, amesema hayo jijini Dar es Salaam alipokuwa akiwaaga vijana hao kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na cha Sokoine cha Kilimo (SUA), wanaokwenda katika nchi za Ujerumani, Sweden na Denmark.

Wanafunzi hao wanakwenda chini ya uratibu wa SUGECO kwa kufadhiliwa na benki ya CRDB.

Amesema weledi na bidii ya kazi, itawaongeza fursa vijana wengine kupata mafunzo hayo, akieleza kuwa baadhi ya Watanzania wanaharibu taswira ya nchi wanapokuwa ughaibuni kwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu au kuacha kufanya kilichowapeleka.

Amesema kupata fursa ya utarajali nje ya nchi kunatengeneza rasilimali watu nchini, ambayo inaweza kuzalisha ajira kwa vijana wengine katika sekta za kilimo, uvuvi na mifugo na ajira za kimataifa.

“Serikali itashirikiana na SUGECO kuandaa mpango wa baada ya utarajali, ili vijana hawa waweze kutumia mafunzo waliyoyapata katika kuchangia maendeleo ya nchi yetu,” amesema.

Aliishukuru Taasisi ya CRDB na SUGECO, kwa kuwapa fursa vijana hao na kusema maandalizi ya rasilimali watu wenye ujuzi, yanahitaji ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na taasisi mbalimbali.

Awali, Kimario alisema baadhi ya nchi ikiwamo Ujerumani, inahitaji vijana wanaofahamu Kijerumani, jambo ambalo ni kikwazo kwa vijana kupata fursa ya kwenda nchini humo.

Amesema SUGECO ina fursa ya kupeleka hadi vijana 1,500 kwenye mafunzo ya vitendo nje ya nchi kila mwaka, ambao wataongeza ujuzi kwa kujifunza kwenye nchi zenye maendeleo makubwa ya viwanda na mashamba ya mifugo, pamoja na teknolojia za kisasa.

Amesema vijana 535 wameshapata fursa ya kwenda kwenye utarajali katika nchi za Ulaya na Marekani 655 tangu mwaka 2022.

“Wakienda wanakaa miezi 12 hadi 18, ni lazima tutengeneze mfumo wa baada ya utarajali ili tuwape mitaji anzia. Tangu tumeanza kushirikiana na CRDB, vijana 40 wamepewa mtaji wa Sh. milioni 460. Tunaona ndani ya muda mfupi, vijana hawa wameanzisha biashara zenye thamani hiyo ya fedha,” amesema.

Amesema chama hicho kimekuwa kikitafuta mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi na wahitimu wa kozi mbalimbali vyuo vikuu na vya kati, hususani za sanyasi ya mimea na chakula udaktari wa mifugo na utalii.

Amesema katika kundi hilo, vijana 13 wanakwenda Ujerumani, 10 Denmark na watatu Sweden.

Mkurugenzi wa wateja wadogo wa CRDB, Bonaventure Paul, amesema benki hiyo imejiandaa kuwezesha vijana na kwamba wametenga fedha kwa ajili ya kujenga biashara za vijana na wanawake.

3