Samia: Tutawania tena nafasi ya Ndugulile WHO

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 09:50 AM Dec 03 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha:Ikulu
Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania itaingia tena katika ushindani wa nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika.

Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam alipoongoza wananchi na viongozi wa kitaifa na kimataifa kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa WHO Kanda ya Afrika, Dk. Faustine Ndugulile. 

Kiongozi huyo aliyefariki dunia Novemba 27 mwaka huu, alichaguliwa kwenye nafasi hiyo Agosti 28 mwaka huu na angeanza majukumu yake Februari 2025.

"Lakini niseme Dk. Faustine katika safari yake hii ya mwisho ameweka heshima kubwa kwa nchi yetu kwa kupata nafasi ile, na niseme kwamba Mungu amechukua amana yake, lakini kwetu sisi ni kwenda mbele.

"Tutaingia tena katika ushindani wa nafasi ile, tutatafuta mtanzania mwenye sifa zinazoweza kushindana na ulimwengu, tutaingia tena na tutaweka nguvu ileile ili kuweka heshima ya nchi yetu. Tunamshukuru sana Dk. Faustine kwa mchango aliotoa kwa taifa.

"Lakini kama tunavyoambiwa kwenye methali za Kiswahili, 'mwanadamu hupati unachotaka, unapata majaaliwa'. Tulichokuwa tunataka ni ndugu yetu huyu atuwakilishe katika shirika lile (WHO), awakilishe Tanzania, na Tanzania kupitia yeye itoe mchango kwa Afrika na dunia kwa ujumla katika fani ya afya lakini kwa Mungu hakutaka twende hivyo, akatupa jaala yake. Wanadamu tunapanga yetu lakini Mungu anapanga ya kwake," Rais alisema.

Watoto wa marehemu Dk. Ndungulile walisema wamepoteza mwanga wao, nguzo na shujaa wao kutokana na vitu alivyokuwa anavifanya kwa familia na jamii.

"Tulipata baba ambaye alikuwa shujaa na aliyetufundisha mambo mengi. Kimwili tumempoteza lakini kiroho tutaendelea kuwa naye," walisema Martha na Melvin.

"Baba alikuwa jasiri, mkarimu, mwenye akili na alipenda watu, nilipata baba... kwangu atabaki kuwa baba bora zaidi," alisema Melvin.

Askofu Msaidizi Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Stephano Musomba aliyeongoza ibada ya kuaga mwili wa Dk. Ndugulile, alisema ili ukumbukwe ni lazima utende mema na kwamba ni vyema watu wajifunze namna ya kuishi na jamii.

"Hakuna atakayekusahau kutokana na matendo yako, hii ni safari ya kujifunza namna ya kuishi na watu, kusaidiana, kuhudumia, safari hii ni darasa ambalo limejaa elimu ya kutosha," alisema Askofu Musomba.

SPIKA TULIA

Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alisema Dk. Ndugulile alikuwa miongoni mwa waliotoa mchango mkubwa katika kumfanyia kampeni kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).

"Ninakushukuru sana Rais Samia kwa bidii kubwa uliyoweka kuhakikisha Dk. Faustine anashinda nafasi hii ambayo pamoja na kwamba ni kama tumekatizwa hivi, lakini imeongeza heshima kwa nchi yetu kuonesha uwezo wa wananchi wa Tanzania ambao unawaongoza.

"Mimi mwenyewe heshima ambayo nimeipata ya kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, Dk. Faustine alikuwa sehemu ya watu ambao walifanya kampeni kwa bidii sana na sina shaka kwa sababu uchaguzi wake ulikuja mwaka mmoja baada yangu, alitumia ule uzoefu ambao wewe Rais ulitoa fursa ya yeye kushiriki katika kampeni, na alitumia uzoefu huo na sasa nchi yetu ikawa imepewa heshima hii.

"Sina shaka Mheshimiwa Rais kuwa jambo hili unalolifanya kwa bidii sana utaendelea kufanya hivyo kwa watanzania wengine wanaojitokeza lakini kwa sababu mimi na Dk. Ndugulile tulikuwa tunatoka upande wa Bunge la Jamhuri, tunakushukuru sana kwa ushirikiano ambao huwa unatupa kila wakati fursa hizi zinapojitokeza," alisema Dk. Tulia.

WAZIRI MKUU 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema amefanya kazi na Dk. Ndugulile na anatambua namna ambavyo amefanya kazi kubwa.

"Tukio hili si dogo, tangu tulipopata taarifa, tulipata mshtuko, binafsi ninatambua namna ambavyo nimefanya naye kazi kwa weledi mkubwa wakati wa utumishi wake, nimeshuhudia namna ambavyo amekuwa akishughulikia matatizo ya watu wa Kigamboni, amekuwa mtumishi katika serikali," alisema Majaliwa.

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Alex Msyoka, alisema wanamkumbuka Dk. Ndungulile kwa ujasiri wake hususani katika kipindi cha kupambana dhidi ya UVIKO-19, ambapo alisimamia taaluma yake kwa ufanisi, na kwamba alikuwa miongoni mwa wanataaluma wa kwanza kuanzisha Mpango wa Kudhibiti Ugonjwa wa UKIMWI Tanzania. 

JOSEPHAT GWAJIMA 

Akizungumza kwa niaba ya wabunge, Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima, alisema Mungu amempatia kila mtu kutimiza kazi yake na kwamba ni vyema kila mtu kuitimiza kwa kuwa muda ni mfupi.

HALIMA MDEE

Mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee alisema, "Mimi kama mwakilishi wa kambi ya watu wachache, ninamfahamu katika shughuli zetu toka mwaka 2010, alikuwa siyo mnafiki, alikuwa kama ana jambo lake kama ni nyeupe atasema nyeupe, kama ni bluu atasema bluu, alitumia muda wake kuwakilisha wananchi, alikuwa anasema kweli tupu, pasipo kujali itamgharimu vipi.

"Tuliomfuatilia alipata ajali za kisiasa kwa sababu ya kuzungumza ukweli, alisimamia anachokiamini, alikuwa mtii. Anatufundisha kwamba hutakiwi kuwa baridi au vuguvugu, inabidi uwe moto utimize ndoto.

"Watoto wanajua ni wa moto na sisi wanasiasa tulijua ni wa moto, hivyo tunaposimama katika jambo la ukweli tunatakiwa tuwe wa moto, ukiwa wa moto unasaidia nchi na kuinua taifa."

Mkurugenzi wa WHO, Kanda ya Afrika, Rebeca Masibiso, alisema Dk. Ndugulile alikuwa mwenye maono kwa ajili ya yale aliyokuwa akifanya, mbunifu, aliwajibika na ndio maana alifanikiwa kushawishi mkutano na kumchagua katika nafasi hiyo WHO.

Waziri wa Afya ya Congo Brazzaville, Gilbert Mukoki, alisema Dk. Ndugulile alivutia hisia za wajumbe wengi wa mkutano wa WHO, na kwa muda mfupi alifanya kampeni kwa ufanisi mkubwa na kuwashawishi wajumbe. Alimtaja "alikuwa mtu makini".

"Wakati tunajiandaa kumpokea kwenye nafasi yake mpya, tukapokea taarifa za kuhuzunisha. Alikuwa na maono ya kufanya mageuzi makubwa kwenye Kanda ya Afrika, maono yake yataendelea kuenziwa na tunaamini yatakuwa mwanga," alisema.

BALOZI NCHIMBI

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema Dk. Ndugulile alikuwa mfano wa kuigwa kwa kizazi cha sasa na kijacho kwa kazi alizofanya na alitoa wito kwa viongozi wote kuiga maisha yake ambayo yalijali maisha ya mtanzania wa kawaida, alijiepusha na ubinafsi na kutanguliza taifa mbele na kwamba ndio maisha ambayo kiongozi anapaswa kuishi.

Dk. Ndugulile alifariki dunia usiku wa kuamkia Novemba 27, mwaka huu India alikokuwa anapatiwa matibabu. Alikuwa mtaalamu wa afya, mwanasiasa mahiri na kiongozi wa mfano aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta za afya, mawasiliano na usimamizi wa kimataifa.

Alizaliwa Machi 31, 1969 katika wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara. Alipata elimu ya juu na kuwa miongoni mwa wataalamu wa kipekee waliochanganya taaluma ya tiba na sheria.

Alipata Shahada ya Udaktari wa Tiba (MD) mwaka 1997 na Shahada ya Uzamili ya Tiba (MMed) mwaka 2001 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Mwaka 2010 alihitimu Shahada ya Uzamili ya Afya ya Umma (MPH) kutoka Chuo Kikuu cha Western Cape, Afrika Kusini, na mwaka 2022 alikamilisha Shahada ya Sheria (LL.B) kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).

SIASA, UONGOZI

Dk. Ndugulile alijiunga na siasa mwaka 2010 alipochaguliwa kuwa Mbunge wa Kigamboni kupitia CCM na aliongoza jimbo lake kwa kujituma, akitekeleza miradi ya kuboresha miundombinu, afya na huduma za kijamii.

Mwaka 2007 hadi 2010 aliwahi kuwa Mshauri Mkazi wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) Afrika Kusini, akitoa msaada wa kiutaalamu kwa nchi nyingine nyingi kama vile Angola, Msumbiji, Tanzania na Rwanda.

Oktoba mwaka 2017, Rais wa Tanzania wa wakati huo, Dk. John Magufuli, alimteua kuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, akisimamia mipango muhimu ya kuboresha huduma za afya, hususani afya ya mama na mtoto.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2020, aliteuliwa kuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari akiongoza kwa ubunifu, na kusisitiza matumizi ya teknolojia kuboresha maisha ya wananchi na kuimarisha uchumi wa kidijitali.

Agosti 27, 2024, Dk. Ndugulile alichaguliwa kuwa Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, nafasi iliyompa heshima kubwa na Tanzania kwa ujumla.

Pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya ya Bunge la Tanzania, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Mabunge ya Kimataifa (IPU) Advisory Group Health na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Mtandao wa Kamati za Afya za Bunge la Afrika (NEAPACOH), ameacha watoto wawili, Martha na Melvin Ndugulile.

Dk. Faustine Ndugulile atakumbukwa kama kiongozi shupavu aliyewakilisha Tanzania kwa heshima katika majukwaa ya kitaifa na kimataifa, akiwa mfano wa kuigwa kwa uadilifu na bidii. Mchango wake katika sekta ya afya, mawasiliano na usimamizi utaendelea kuishi milele.