CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida kimekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuondokana na fikra kwamba katiba mpya ndio itakiwezesha kupata ushindi katika Uchaguzi Mkuu mwakani.
Katibu wa CCM Wilaya ya Ikungi, Joshua Mbwana, amesema chama hicho cha upinzani kitambue kuwa wanaopiga kura ni wananchi na si katiba ambayo imekuwa inapigiwa kelele na viongozi wakuu wa CHADEMA wakidai Katiba mpya.
Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ushindi ambao chama hicho kimeupata wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 27, mwaka huu.
"Nimemsikia kaka yangu Tundu Lissu akisema uchaguzi unaokuja 2025, kama hakuna Katiba mpya ni bure kwenda kwenye huo uchaguzi.
"Niwaambie katiba haipigi kura, kinachopiga kura ni watu, watu hawa waliomwelewa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kutokana na miradi mingi aliyoleta, ndio hawa hawa watakaopiga kura Uchaguzi Mkuu mwaka 2025," alisema.
Mbwana alipoulizwa iwapo Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Lissu, akijitokeza kugombea ubunge mwakani katika wilaya hiyo, alisema CCM inamkaribisha kama ana nia hiyo.
Hata hivyo, alidai mwanasiasa huyo atapata aibu kwa kupata kura chache kama ilivyotokea katika kijiji cha Mahambe alikozaliwa; kijiji na vitongoji vyote vimechukuliwa na CCM wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
"Mimi ninataka kumwambia, kama Lissu ana wazo hilo la kutaka kuja kugombea ubunge asipoteze muda, atafute shughuli nyingine ya kufanya au akatafute sehemu nyingine ya kwenda kugombea maana atapata aibu nyingine tena," alidai.
Katibu huyo alisema kuwa wilayani Ikungi, kuna kata 28, viijiji 101, vitongoji 539. Kati ya vitongoji vyote, kitongoji kimoja hakikufanya uchaguzi kutokana na mgombea wa CHADEMA kufariki dunia siku mbili kabla ya uchaguzi.
Alisema kati ya vitongoji 538, CCM imeshinda vitongoji 536, vitongoji viwili vimechukuliwa na upinzani.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED