WAKAZI wa Mtaa wa Mustafa Kata ya Pugu Wilaya ya Ilala wamehakikishiwa kuondolewa adha ya kwenda umbali mrefu kufuata huduma ya afya na elimu ambayo ilikuwa changamoto kubwa kwa wakazi hao.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo katika mkutano wa hadhara na wananchi wa mtaa huo. Mpogolo amesema Serikali imedhamiria kumaliza changamoto zote za elimu kwa wanafunzi wanaokwenda kusoma nje ya mitaa yao wanaoishi.
Amesema Serikali kupitia Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam imetenga fedha kwa ajili ya kujenga shule katika eneo hilo ili kupunguza kero ya watoto kusoma katika mitaa mingine.
Amebainisha kuwa hadi ifikapo Januari mwakani mategemeo makubwa wanafunzi waanze kusoma mitaa husika na tayari ameshamuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri jiji kupeleka wakandarasi wa michoro katika eneo la ujenzi ili kuanza ujenzi wa shule hiyo ya msingi.
Aidha amefafanua kuhusu changamoto ya dampo la Pugu kuwa serikali kwa imeandaa mpango shirikishi kwa taasisi na kampuni kubadili mtazamo wa taka badala ya kukusanywa zianze kuchakatwa na kufungua fursa ya ajira.
Ameeleza kuwa yapo madampo yaliyobadilika katika majiji kwa kuanza kuchakata taka ili zitumika kwa mbolea, chakula cha mifugo na malighafi katika vifaa vya ujenzi.
Pamoja na kuzungumzia ilo amewatoa hofu wananchi wa mtaa huo juu ya vivuko na barabara ambazo zimekua changamoto kwa kuwaeleza fedha zinazokusanywa na Halmashauri zaidi ya Shilingi billioni 130 kwa mwaka .
Kuhusu suala la ukuta wa dampo kuanguka ameeleza tayari serikali imepanga kuanza ujenzi wa ukuta na kuweka mifereji ya maji ili kusiende kwenye makazi ya wananchi. Katika mkutano huo Mpogolo amempongeza Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Mustafa kwa kuwapatia sare walinzi shirikishi, na kutoa rai kwa mitaa mingine kuiga mfano huo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED