Nane wajitosa kumng'oa Ndugai Kongwa

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 04:03 PM Jun 28 2025
Nane wajitosa kumng'oa Ndugai Kongwa
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Nane wajitosa kumng'oa Ndugai Kongwa

Job Ndugai, ambaye amekuwa Mbunge wa Jimbo hilo tangu mwaka 2000 na kuongoza kwa kipindi cha miaka 25 mfululizo alitangaza kurudi tena kwa ajili ya kugombea uchaguzi Mkuu 2025 kupitia CCM.

Saa nne mara baada ya kufunguliwa kwa pazia la uchaguzi wa kura za maoni ndani ya CCM, watu nane wamejitokeza Jimbo la Kongwa. Chama Cha Mapinduzi kimefungua pazia hilo leo Jumamosi Juni 28,2025 ambalo litadumu hadi Julai 2,2025.

Jimbo la Kongwa kwa sasa linaongozwa na Spika Mstaafu Job Ndugai ambaye amedumu tangu 2000 alipolichukua kutoka kwa Gidion Senyagwa. Hata hivyo ushindani mkali unatajwa kuwa kati ya Ndugai na Seif ambao kwa muda mrefu walikuwa marafiki lakini wanawania kiti kimoja huku Seif akitangaza silaha yake ni Mungu.

Mapema leo baadhi ya wananchi wa Kongwa walikuwa wamekusanyika pembeni mwa Ofisi za CCM wakimsubiri Deus Seif ambaye hata hivyo alipobaini kuna wananchi wanamsubiri aliamua kuingilia mlango mwingine akiwa peke yake akieleza anakwepa kusindikizwa.

Wakati wa kutoka pia aliondoka kwa namna ya kutoonekana ambapo baadhi ya wananchi walisema watabaki hapo lengo ni kutaka washuhudie Seif akichukua fomu na kurudisha. Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) amechukua fomu akiwa mtu wa tatu akitanguliwa na Philip Chiwanga na Aloyce Mbujilo.

Baadae wamekuja Henry Mwatwiza, Elias Mdao, Dk Simon Ngatunga na Sehewa Sabugo.Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu hizo, Seif amezungumza maneno mawili akisema "Namshukuru Rais Samia kuweka uwanja huru kwa wagombea, lakini namtegemea Mungu kwa kila jambo," 

Wagombea hao walikabidhiwa fomu na Katibu wa CCM Wilaya ya Kongwa Joyce Mkaula ambaye aliwaelekeza kwenda kuzilipia Sh.500,000 kila mmoja na chama kiligoma kuchukua fedha mkononi.