Jina la Amadeus Shayo laibuka Vunjo kuelekea Uchaguzi 2025

By Allan Isack , Nipashe
Published at 05:10 PM Jun 27 2025
Mwanasheria wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Amadeus Shayo
Picha: Mptandao
Mwanasheria wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Amadeus Shayo

Wakati joto la kisiasa likianza kupanda taratibu kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, Jimbo la Vunjo limeanza kushuhudia mijadala mizito kuhusu mwelekeo wa uongozi na aina ya viongozi wanaotarajiwa kulitumikia jimbo hilo kwa miaka mitano ijayo.

Katika hali isiyotarajiwa na wengi, jina la Mwanasheria wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Amadeus Shayo, limeanza kutajwa mara kwa mara katika vikao vya kijamii, mijadala ya vijana na hata maoni ya wazee wa kimila, kama mmoja wa watu wenye sifa zinazohitajika katika zama za sasa za uongozi.

Shayo, ambaye ni mbobezi wa Sheria za Uchumi wa Kimataifa, anatajwa kuwa na sifa za kipekee za uongozi na dhamira ya kweli ya kulitumikia taifa kupitia uwakilishi wa wananchi wa Vunjo bungeni.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa wa ndani ya jimbo hilo, endapo Shayo atajitokeza kugombea ubunge, Mbunge anayemaliza muda wake, Dk. Charles Kimei, anaweza kukumbana na upinzani mkali kutokana na ushawishi mkubwa alionao Shayo na namna anavyokubalika kwa wananchi.

Akizungumza na Nipashe, mmoja wa wakazi wa Vunjo, Sigfrid Kimario, alisema:
“Wanasheria wa Serikali walimtambua kuwa ni kiongozi wa kipekee kwa kumpa heshima ya kuwa Rais wao wa kwanza kupitia Public Bar Association. Huu ni ushahidi kuwa anaaminika, ana uwezo na dhamira ya kweli ya kuliletea taifa maendeleo.”

Aliongeza kuwa sasa ni wakati muafaka kwa Shayo kuchukua fomu na kugombea ubunge wa Jimbo la Vunjo ili kuwatumikia wananchi na kuwa sauti yao bungeni.

Naye Albert Tarimo alisema jimbo hilo linahitaji kiongozi anayeweza kujenga hoja bungeni, mwenye upeo wa kimataifa lakini pia anayeelewa changamoto za wananchi wa kawaida:
 “Kwa miaka mitano iliyopita, tumekuwa na uwakilishi usio na tija. Tunahitaji mtu kama Shayo, mwenye dira ya kweli ya maendeleo.”

Akimwelezea zaidi, Tarimo alieleza kuwa Shayo ni msomi na wakili mahiri wa Mahakama Kuu, ambaye ameonyesha mwelekeo wa kitaifa na mtazamo wa kimataifa kuhusu maendeleo jumuishi kupitia mfumo wa kisheria.

Kupitia andiko lake la PhD katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand, Afrika Kusini, Shayo anachambua kwa kina uhusiano kati ya sheria na maendeleo ya uchumi – hasa katika usimamizi wa rasilimali kama madini kama kichocheo cha ustawi wa taifa.

Amefanikiwa pia kupata ufadhili kutoka Serikali ya China kupitia mpango wa Youth of Excellence kwa ajili ya kusomea Shahada ya Umahiri katika Sheria za Uchumi wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha East China University of Political Science and Law – jambo linaloonyesha namna anavyothaminiwa kimataifa.

Shayo pia alihitimu Shahada ya Sheria (LL.B) kwa heshima kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na kwa sasa ni Rais wa Kwanza wa Public Bar Association (PBA) – chama cha wanasheria wa Serikali kinacholenga kulinda maslahi ya umma kwa weledi na uzalendo.

Aidha, Kimario alisisitiza kuwa uzoefu wake wa kimataifa na kujitolea kwake kwa taifa ni ushahidi kuwa mbali na kuwa msomi, Shayo anazo sifa za kuwa kiongozi mtarajiwa.

“Endapo msomi huyu ataamua kugombea, atakuwa tishio – si kwa ubabe wa kisiasa, bali kwa kusukuma ajenda ya maendeleo yenye msingi wa maarifa, maadili na uzalendo.”

Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa, ikiwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitaendelea kuwekeza katika kizazi kipya cha viongozi vijana, wachapakazi, waaminifu na wasomi, basi Amadeus Shayo ana nafasi kubwa kuwa hazina ya kisera na kichocheo cha uongozi mpya wa taifa – unaojenga msingi wa leo na kesho.