RC Chalamila akagua maendeleo ujenzi wa madaraja

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 03:49 PM Jun 27 2025
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila
Picha: Imani Nathaniel
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amefanya ziara ya ukaguzi katika maeneo ya ujenzi wa madaraja ya Kigogo, Jangwani na Mkwajuni. Katika ziara hiyo, Chalamila amewataka wananchi kuwa watulivu na kufuata utaratibu utakaowekwa na mamlaka husika wakati wa ujenzi huo unaoendelea.

Amesema kuwa ujenzi wa Daraja la Jangwani umeanza rasmi na kufikia asilimia 7 ya utekelezaji, huku akieleza kuwa daraja hilo linatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka miwili. Mradi huo unakadiriwa kugharimu Shilingi bilioni 97, ambapo tayari Shilingi bilioni 14 zimetolewa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ametoa wito kwa mkandarasi anayejenga daraja hilo kuhakikisha anakamilisha kazi kwa wakati ili kusaidia kupunguza changamoto ya msongamano wa magari. Aidha, amewataka wananchi wa Ilala kufuata maelekezo yatakayotolewa na askari wa usalama barabarani kwa lengo la kurahisisha mzunguko wa magari kipindi chote cha ujenzi.

Mradi wa Daraja la Kigogo unagharimu Shilingi bilioni 11, huku ule wa Mkwajuni ukiwa na gharama ya Shilingi bilioni 17. Serikali inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo muhimu kwa maendeleo ya miundombinu na kupunguza adha ya foleni kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.