Kabalika aeleza mafanikio ya miaka mitano Kata ya Sandali
By
Grace Mwakalinga
,
Nipashe
Published at 12:24 PM Jun 27 2025
Picha: Mtandao
Kabalika aeleza mafanikio ya miaka mitano Kata ya Sandali
Wakati Bunge la 12 likihitimishwa rasmi leo na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, baadhi ya viongozi kutoka maeneo mbalimbali nchini wameeleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wa Bunge hilo.
Mmoja wa viongozi hao ni aliyemaliza muda wake, Diwani wa Kata ya Sandali, Wilaya ya Temeke, Christopher Kabalika, ambaye amesema kuwa Bunge hilo limechangia kwa kiasi kikubwa katika upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu na afya katika kata hiyo.
Kabalika amesema kuwa kupitia Mradi wa BOOST, kiasi cha Shilingi milioni 139 kilitumika kujenga madarasa sita katika Shule ya Msingi Sandali pamoja na matundu matano ya vyoo. Hatua hiyo imesaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani na kuwaondolea adha ya kupokezana madarasa.
Aidha, katika Shule ya Msingi Vetenari, walipokea Shilingi milioni 200 zilizotumika kujenga madarasa sita, kukarabati madarasa manane, na kujenga matundu 12 ya vyoo vya wanafunzi. Pia, kupitia ushirikiano na wadau wa maendeleo, walifanikiwa kujenga matundu manne ya vyoo kwa ajili ya walimu kupitia mradi wa WASH.
“Katika Shule ya Sekondari Temeke, tulitumia Shilingi milioni 180 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu, ikiwa ni pamoja na ukarabati wa madarasa ya Kidato cha Tano na ujenzi wa matundu nane ya vyoo,” ameongeza Kabalika.
Kuhusu sekta ya afya, Kabalika amesema kumekuwa na maendeleo makubwa katika utoaji wa huduma za matibabu katika Kata ya Sandali, ambapo Zahanati ya Sandali sasa inatoa huduma bora na za uhakika kwa wananchi.
Amesema kuwa serikali inaendelea na ujenzi wa Kituo Kikubwa cha Afya katika kata hiyo, ambapo hadi sasa zaidi ya Shilingi milioni 500 zimetolewa kwa ajili ya kuanza ujenzi huo, huku Shilingi milioni 230 zikitolewa kwa ajili ya fidia kwa wananchi waliopisha mradi huo.
“Tunajivunia mafanikio haya katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa serikali. Ufaulu wa wanafunzi umeongezeka kwa sababu sasa wanasoma katika mazingira bora, na wananchi wanapata huduma za afya za uhakika kutokana na usimamizi mzuri wa Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, na Mkurugenzi wa Halmashauri, Jomary Mrisho Satura,” amesema Kabalika. 1