"Ikiwa ni Ruto lazima aondoke, namna gani mnataka niondoke…”

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 08:47 AM Jun 28 2025
Rais William Ruto
Picha: Mtandao
Rais William Ruto

RAIS wa Kenya, Dk. William Ruto, amesema wale wanaoandamana wakimtaka ajiuzulu wanapuuza Katiba ya nchi, ambayo inaeleza wazi kuhusu muhula wa urais.

“Hauwezi kuwa na zaidi ya hapo, kwa hiyo ni nini hiki kinachozungumzwa sana kuhusu muhula? Katiba tayari imeelekeza kuhusu hilo, sasa tutafute suluhisho la changamoto zetu. Suluhisho halipo kwenye muhula, lipo kwenye mikakati na mipango,” amesema Rais.

Rais Ruto alitumia fursa hiyo kuzungumzia kauli ya “wantam” (muhula mmoja tu) inayolenga kuwahamasisha Wakenya wasimchague tena mwaka 2027, akisema wale wanaoendeleza ujumbe huo hawatoi suluhisho mbadala kwa Wakenya.

“Ikiwa ni ‘Ruto lazima aondoke’, niambieni ni namna gani mnataka niondoke. Tuwe wa kweli na wawazi. Mnapomaanisha Ruto lazima aondoke, mnamaanisha nini? Niondoke vipi?

“Kwa sababu tuna Katiba, sivyo? Ikiwa mnataka Ruto aondoke, ushauri wangu ni rahisi: tafuteni mpango bora zaidi. Washawishini Wakenya kuwa mna mpango bora zaidi.”

Rais amezungumza hayo katika Ukumbi wa Kimataifa wa Kenyatta (KICC), akiwaongoza Wakenya kuadhimisha Siku ya Biashara Ndogo na za Kati Duniani, mwaka 2025.

“Ikiwa mtaweza kutushawishi kwamba mna mpango bora kuliko wangu na Wakenya wakawachagua kwa msingi wa mpango huo, basi naweza kuondoka nikajikita kwenye kilimo na kusaidia katika kuhakikisha usalama wa chakula, ikiwa mna mpango bora zaidi. Lakini tafadhali, msiiangamize nchi, hatuna nchi nyingine ya kwenda,” ameongeza.

“Vurugu na fujo havitawapeleka madarakani. Mnataka Ruto aondoke? Fanyeni jambo la heshima, tengenezeni mpango bora kuliko wangu.”

Anasema maandamano yaliyosababisha vurugu jijini Nairobi na maeneo mengine hayakuwa ya amani, bali yalikuwa ni vitendo vya makusudi vya ghasia, uharibifu wa mali na kuhujumu uchumi wa taifa.

“Kile tulichoshuhudia hakikuwa maandamano ya amani. Ilikuwa ni fujo zilizopangwa, ilikuwa ni vurugu, uharibifu na hujuma ya kiuchumi. Tukiite kwa jina lake halisi.”

Akiwahutubia wapinzani wake wa kisiasa, Rais amewasihi watafute kura kwa kuwasilisha mipango bora kwa wananchi, badala ya kutumia maandamano kama chombo cha kuibana nchi.

Rais Ruto pia amesisitiza haja ya kuwaongoza Wakenya katika njia sahihi na kuepuka kuunga mkono matukio au harakati zinazoweza kuipeleka nchi katika vurugu.

Akiwaonesha huruma familia zilizopoteza wapendwa wao na wale waliopoteza biashara zao, Rais amemwagiza Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, kuwatafuta na kuwachukulia hatua wale wote waliokuwa chanzo cha fujo hizo.

“Natarajia Inspekta Jenerali wa Polisi na taasisi zote husika za usalama waendeleze uchunguzi wa haraka, wa kina na wa haki. Wale waliotekeleza vurugu, uporaji na uharibifu lazima watambuliwe, wafuatiliwe na wafikishwe kwenye mkono wa sheria kwa haraka na kwa ufanisi.”

Ameonya viongozi kuhamasisha vurugu na uharibifu wa biashara, akisema ikiwa hali hiyo itaachwa iendelee, itasambaa kote nchini na hakuna atakayepona.

Chanzo: Mtandao