NACTVET yatoa mafunzo kwa Maafisa Udahili na Mitihani Vyuo Vikuu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:24 PM Jun 27 2025
Mkurugenzi wa Udahili, Utahini na Utunuku, Dk. Marcelina Baitilwake.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Udahili, Utahini na Utunuku, Dk. Marcelina Baitilwake.

Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limeandaa semina maalum kwa Maafisa Udahili na Mitihani kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ubora wa elimu na usimamizi madhubuti wa taratibu, kanuni, sheria na miongozo inayosimamia udahili na mitihani kwa ngazi ya Astashahada na Stashahada.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa NACTVET katika ufunguzi wa semina hiyo leo,  Juni 27, 2025, mjini Morogoro, Mkurugenzi wa Udahili, Utahini na Utunuku, Dk. Marcelina Baitilwake, amesema lengo la semina hiyo ni kuwawezesha Maafisa hao kupata uelewa wa kina kuhusu kanuni, taratibu na sheria za udahili na mitihani kama zilivyoainishwa na Baraza.

Dk. Baitilwake amesema changamoto nyingi zinazowakabili wanafunzi katika vyuo mbalimbali hutokana na kutokuzingatiwa kwa miongozo ya Baraza, hivyo semina hiyo inalenga kupunguza changamoto hizo, hasa kwenye masuala ya Udahili, Matokeo na Namba ya Utambuzi wa Tuzo (AVN).

Kwa upande wao, washiriki wa semina hiyo wameipongeza NACTVET kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo wamesema yamewajengea uelewa mpana kuhusu majukumu yao na mbinu bora za kuyatekeleza kwa ufanisi, kwa kuzingatia miongozo ya Baraza.

Semina hiyo ya siku tatu ilianza tarehe 26 Juni 2025 na inatarajiwa kufikia tamati kesho tarehe 28 Juni 2025.