Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa imezindua rasmi Mpango Kabambe wa Maji, Usafi wa Mazingira na Usafi Binafsi (WASH Master Plan), kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo, katika hafla iliyofanyika leo jijini Dodoma.
Mpango huu wa kimkakati unalenga kipindi cha mwaka 2024 hadi 2036, na unakusudia kuhakikisha upatikanaji wa huduma endelevu na jumuishi za maji safi, usafi wa mazingira na usafi binafsi kwa wakazi wote wa Wilaya ya Mpwapwa.
Uzinduzi huo umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Water For People Tanzania, na umehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Henry Chisute, Mkurugenzi wa Ubora wa Maji kutoka Wizara ya Maji, aliyemwakilisha Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Dk. Sophia Kizigo, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya Mwanahamisi Ally, Mkurugenzi Mkazi wa Water For People Tanzania Dk. Happiness Willbroad, Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mha. Wolta Kirita, na wadau wengine kutoka sekta ya WASH ndani na nje ya mkoa.
Mpango huo umetayarishwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya Water For People, Halmashauri ya Mpwapwa, RUWASA, na Mamlaka ya Maji Mpwapwa (MPWUWSA). Lengo kuu ni kuboresha utoaji wa huduma za maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi kwa kiwango cha hali ya juu, kwa malengo ya kufanikisha upatikanaji wa huduma hizo kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2036.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mgeni Rasmi Mkurugenzi wa Ubora wa Maji kutoka Wizara ya Maji, Henry Chisute amesisitiza umuhimu wa matumizi bora ya maji na kuhakikisha mpango huu unatekelezwa kwa vitendo:
"Tunakumbwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji; hivyo, pale maji yanapopatikana, ni muhimu tuyatumie kwa ufanisi. RUWASA na Halmashauri ya Mpwapwa wahakikishe mpango huu hautabaki kwenye makaratasi bali utekelezwe kwa vitendo kama sehemu ya kutimiza malengo ya kitaifa."
Ameendelea kusisitiza kuwa Halmashauri nyingine nchini nazo zitengeneze mipango mikuu ya maji na usafi inayokwenda sambamba na sera ya maji ya mwaka 2002 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2025, pamoja na Dira ya Taifa 2025 hadi 2050. Amefichua kuwa katika bajeti ya mwaka 2025/2026, kila wilaya imeelekezwa kutenga fedha kwa ajili ya maandalizi ya mipango hii, ambayo itahitimishwa kwa kuandaliwa kwa Mpango Mkuu wa Taifa wa Sekta ya Maji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mha. Wolta Kirita amethibitisha kuwa taasisi hiyo imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 6 kwa ajili ya kusaidia uandaaji wa Mipango ya WASH katika wilaya 123 kati ya 128, huku Mpwapwa ikiwa ni miongoni mwa wilaya nne za awali tayari zenye mipango hiyo. Alihimiza wadau wengine kuunga mkono juhudi hizi.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Dk. Sophia Kizigo, ameeleza:
"Nawapongeza Water For People kwa kushirikiana nasi tangu mwanzo. Mpango huu umebuniwa kwa ushirikiano mkubwa, jambo linaloongeza uwezekano wa mafanikio. Mpango unalenga kufikia asilimia 65 ya upatikanaji wa maji ya bomba karibu na jamii ifikapo 2026, lakini tunaamini tunaweza kufikia asilimia 80. Pia lengo la kuongeza kaya za vijijini zinazojiunganishia maji majumbani kutoka asilimia 4 hadi 25 ifikapo 2026 ni la kishujaa."
Mkurugenzi Mkazi wa Water For People Tanzania, Dk. Happiness Willbroad, ameeleza dhamira ya shirika hilo kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali:
"Huu ni mwanzo tu wa safari yetu. Water For People itaendelea kuwepo Mpwapwa kuhakikisha angalau asilimia 95 ya familia zinapata huduma endelevu za maji safi; asilimia 95 ya vituo vya kutolea huduma za afya na shule vinapata huduma bora za WASH; na asilimia 90 ya familia zinapata huduma bora za usafi wa mazingira na usafi binafsi."
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED