Majaliwa: Rais Samia aliifanya kazi yangu kuwa nyepesi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:25 PM Jun 26 2025
Rais Samia Suluhu Hassan
Picha: Mtandao
Rais Samia Suluhu Hassan

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake akisema wakati wote amekuwa akimpatia maelekezo yenye tija na kuifanya kazi yake kuwa nyepesi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake akisema wakati wote amekuwa akimpatia maelekezo yenye tija na kuifanya kazi yake kuwa nyepesi.

Pia amesema hana shaka kwamba wabunge wote watakubaliana nae kuwa ustahimilivu wa kiongozi huyo wa taifa umekuwa faraja kwa wasaidizi wake, watumishi wote wa umma na Watanzania kwa ujumla.

Waziri Majaliwa ameyasema hayo leo katika hutuba yake bungeni jijini Dodoma wakati akihitimisha mkutano wa 19 wa bunge la 12, akisema; "wakati wote Rais Samia amekuwa nguzo ya kuimarisha mshikamano na umoja wa kitaifa."

"Niwashukuru pia wabunge wenzangu kwa ushirikiano, mshikamano mlionipa wakati wote nikiwa natekeleza jukumu langu la kiongozi wa shughuli za serikali bungeni. Sitawasahau na sitasahau upendo wenu kwangu Inshaalah Mwenyezi Mungu atawajaalia kila lenye kheri katika kila jambo lenu," amesema Majaliwa

Kadhalika, Waziri Majaliwa amewashukuru wana Ruangwa kwa kumuunga mkono na kunipatia ushirikiano katika kipindi chote alipokuwa akitekeleza majukumu yake kama waziri mkuu.

"Ninatambua wakati mwingi nimekuwa nje ya jimbo nikilitumikia taifa lakini wana Ruangwa wameendelea kuniunga mkono. Ninamuomba Mwenyezi Mungu azidi kuimarisha mshikamano uliopo kati yetu sote. Ninaomba kuwajulisha kuwa ninakuja kuchukua fomu ya kuomba ridhaa yenu tena," amesema Majaliwa.