CCM yaeleza sababu kuzuia shamrashamra uchukuaji, urejeshaji fomu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:38 PM Jun 26 2025
Katibu wa NEC Organaizesheni, Issa Haji Ussi
Picha: Mtandao
Katibu wa NEC Organaizesheni, Issa Haji Ussi

Chama Cha Mapinduzi kimeeleza sababu za kuzuia shamrashamra za matarumbeta,ngoma,wapambe na pilipiki katika kuchukua na kurudisha fomu za ubunge na udiwani.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na Katibu wa NEC Organaizesheni, Issa Haji Ussi kuhusu mwongozo wa na maelekezo kuhusu utaratibu wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa wanachama.

Amesema lengo la zuio ni kutoka na muhimu wa mchakato kwa chama katika kuwaunganisha wanachama wake ili kulinda misingi ya umoja, upendo, ushirikiano, mshikamano.

"Ili kusimamia misingi hiyo, inaelekezwa kwamba:- Ni, marufuku kwa mwanachama yeyote kualika kundi la wapambe kumsindikiza kwenda CCM kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea."amesema.


"Ni marufuku kwa mwanachama kuandaa msafara wa magari, pikipiki, baiskeli, ngoma na matarumbeta ya kumsindikiza kwenda CCM kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea, vitendo hivyo vinaleta viashiria vya makundi na mpasuko ndani ya Chama, havipaswi kufanywa na mwanachama yeyote."


Ussi amesema CCM inaelekeza usimamizi wa karibu mchakato huu, kuhakikisha kila mwanachama anaheshimu na anafuata maelekezo haya. 

"Mwanachama yeyote atakayepuuza na kukiuka maelekezo haya, hatua za kinidhamu zichukuliwe ipasavyo, kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili dhidi yake, bila upendeleo wala uonevu, ikiwemo ni pamoja na kumuondolea sifa za kuteuliwa kuwa mgombea.


"Maelekezo haya mnatakiwa kuyafikisha haraka sana kwa makatibu wote wa wilaya, na kata ili waweze kuwajulisha wanachama wanaokusudia kuchukua fomu za kugombea, nao waweze kufahamu juu ya katazo hili."