Watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye Magereza kwa Tanzania Bara na Vyuo vya Mafunzo kwa Tanzania Zanzibar wamekumbushwa kutunza vifaa.
Mjumbe wa INEC, Balozi Omar Ramadhan Mapuri ametoa wito huo mkoani Dodoma leo, akifunga mafunzo kwa waratibu, waandishi wasaidizi na waendesha vifaa vya Bayometriki kwa magereza ya Tanzania Bara.
"Ikumbukwe kuwa mafunzo na maelekezo mliyopewa ni zana muhimu za kuwawezesha kutekeleza kwa ufanisi majukumu yenu. Hivyo, mnatakiwa kuyafahamu vizuri na kuyafuata. Someni kwa makini vitabu vya maelekezo mlivyopatiwa ili kazi yenu ifanyike kwa usahihi na kutunza vizuri vifaa vya kazi,” amesema Mapuri.
Akifunga mafunzo kama hayo kwa watendaji wa vyuo vya mafunzo yaliyofanyika visiwani Zanzibar, Mjumbe wa tume hiyo Jaji wa Mahakama Kuu, Asina Omari aliwasisitiza watendaji hao pia kutunza vizuri vifaa vya uboreshaji wa daftari hilo.
"Mnasisitizwa kuzingatia kwa umakini utunzaji wa vifaa vya uandikishaji kwa kuwa vifaa hivi vimenunuliwa kwa gharama kubwa. Kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa hivi kutasababisha athari kubwa ya vifaa hivyo muhimu kwa taifa,” amesema Jaji Asina.
Amesema ni muhimu pia watendaji hao juu kuzingatia muda sahihi wa kufungua na kufunga vituo vya kuandikisha wapigakura na kutumia lugha nzuri kwa wale watakaowahudumia vituoni.
Mafunzo hayo ya siku tatu yamefanyika sambamba na mafunzo ya watendaji wa vyuo vya mafunzo kwa upande wa Tanzania Zanzibar ikiwa ni maandalizi ya kuandikisha na kuboresha taarifa za mahabusu, wafungwa na wanafunzi waliohukumiwa kifungo chini ya miezi sita.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na tume hiyo, zoezi la uboreshaji wa daftari kwenye Magereza na Vyuo vya Mafunzo litafanyika kwa siku saba kuanzia Juni 28 hadi Julai 4 mwaka huu, kwa kuandikisha mahabusu na wafungwa walihukumiwa kifungo chini ya miezi sita.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED