Baadhi ya wanawake Dar wafanya dua kuliombea Taifa amani
By
Pilly Kigome
,
Nipashe
Published at 02:20 PM Jun 24 2025
Picha:Mpigapicha Wetu
Baadhi ya wanawake Dar wafanya dua kuliombea Taifa amani
Baadhi ya wanawake Mkoa wa Dar es Salaam wamefanya dua maalumu ya kuwaombea viongozi wakuu wa nchi Rais Dk.Samia Suluhu Hassan na Rais Dk.Hussein Mwinyi na kuliombea Taifa liendelee kuwa na uhuru na amani iliyopo.
Wanawake kutoka makundi mbalimbali waliungana wakiwemo wale Mahujaji waliotoka kuhiji Makka, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania(BAKWATA), Umoja Wa Wanawake Tanzania(UWT), Taasisi za dini, wananchi kwa pamoja walifanya dua hiyo katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa Dua hiyo Sabahi Chondoma aliviambia vyombo vya habari kuwa wameamua kufanya dua hiyo kwa lengo la kuiombea nchi iendelee kuwa na amani katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu kusiwe na migogoro wala machafuko yoyote.
“Rais Samia na Rais Mwinyi ndio viongozi wakuu wa nchi hivyo tumewaombea waweze kuliongoza vyema taifa bila wao sisi watu wa chini si lolote si chochote wao ndio watakaoweza kuilinda nchi hii hivyo ni lazima tuwaombee wao na wasije watu wabaya wakawafikia” amesema
Amesema wametafakari kwa kina wao kama wanawake wameona hawana pa kukimbilia kuomba msaada isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu pekee kuiombea nchi yetu amani.
Hajat Maryamu Dedes mmoja wa mahujaji waliorudi kutoka Makka aliviambia vyombo vya habari kuwa wanawake ni jeshi kubwa tukiungana kwa pamoja kuitafuta amani ya nchi na kumlilia Mwenyezi Mungu basi nchi itaendelea kuwa na amani na utulivu na nchi itaepukana na migogoro ambayo itakuja kuibomoa nchi.
Amesema wanapigania amani ya nchi usiku na mchana kwakuwa katika mitandao ya kijamii kuna mambo mengi yanayoendelea ambayo yana viashiria wa uvunjifu wa amani hivyo ni wajibu wao kuliombea Taifa.
Neema Maumba kutoka wanawake Bakwata amesema hawana sababu ya kutokumuombea dua Rais Dk.Samia Suluhu na Dk.Hussein kwakuwa ni viongozi shupavu na wameweza kudumisha amani kwa kipindi chote cha miaka mitano.
Pia wameweza kuwaletea maendeleo wananchi katika kila sekta mbalimbali ikiwemo kuboresha na kuongeza vituo vya afya, kuboresha elimu, miundombinu na kuwawezesha wanawake katika kukuza uchumi kwa kuwapa mikopo isiyo na riba ili wajikomboe kiuchumi.
“Tunachoweza kusema wanawake wenzangu tunaenda katika uchaguzi basi tuweze kuchagua viongozi waadilifu na watakaodumisha amani ya nchi” amesema 2