Makalla: Watanzania mitandaoni wameikubali 'Oktoba Tunatiki'

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 06:49 PM Jun 23 2025

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla.
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla, amesema kila wakiangalia katika mitandao ya kijamii ni ‘Oktoba Tunatiki’ kwa sababu alizozieleza kuwa Watanzania wamekataa No Reforms No Election, wanataka kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo.

Ameyasema hayo leo Juni 23,2025,  katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mpwapwa mjini, mkoani Dodoma, katika ziara yake ya siku tatu aliyoianza ikihusisha mkoa huo na Singida.

Amesema wanakwenda katika uchaguzi lengo likiwa ni kushiriki na kushinda kwa kishindo, akihamasisha wananchi kutunza vichinjio vyao hadi muda utakapofika.

“Msiwasikilize wanaosema No Reforms No Election kwa kuwa wana mgogoro katika chama chao, hivyo muda wa kupiga kura ukifika mkashiriki uchaguzi kwa sababu matayarisho yake yanaendelea vizuri.

“Msingi wa matumaini yetu ni namna wananchi wa Watanzania mlivyotuamini kwa ushindi wa asilimia 98 katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,” amesema.