Madaktari 43 wanaojulikana kama Madaktari Bingwa wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan wamewasili mkoani Shinyanga kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi wa mkoa huo.
Madaktari hao wamewasili leo, Juni 23, 2025, na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, kabla ya kusambazwa katika halmashauri zote sita za mkoa huo ambapo watatoa huduma kwa muda wa siku sita hadi Juni 28.
Akizungumza katika mapokezi hayo, Macha amempongeza Rais Samia kwa kuendelea kujali afya za wananchi wake, akibainisha kuwa pamoja na kuboresha huduma za afya, pia ameendelea kuleta madaktari bingwa na kuweka kambi kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.
“Natoa wito kwa wananchi wote wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi kupata huduma za kibingwa kutoka kwa madaktari hawa waliopo katika halmashauri zote sita,” amesema Macha.
Kiongozi wa madaktari hao kutoka Wizara ya Afya, Grace Mariki, amesema watahudumu mkoani Shinyanga kwa siku sita na wamekuja na madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, watoto, upasuaji, magonjwa ya ndani, kinywa na meno, ganzi, pamoja na masikio, pua na koo.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Yudas Ndungile, amesema ujio huo wa madaktari bingwa pia utakuwa fursa ya kuwajengea ujuzi wa kibingwa watumishi wa afya wa mkoa huo.
Nao baadhi ya madaktari hao, akiwemo Joackim Kisaka, wamesema wako tayari kutoa huduma kwa wananchi wa mkoa huo na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kufaidika na huduma hizo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED