Serikali yatoa milioni 669 kujenga Kituo cha Afya Madilu, Ludewa

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 05:42 PM Jun 23 2025
Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas.

Serikali imetoa shilingi milioni 669 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Madilu, wilayani Ludewa, mkoani Njombe, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha huduma za afya kwa wananchi wa maeneo ya pembezoni.

Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas, amebainisha hayo alipokuwa akizungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara iliyofanyika kwenye vijiji vya Ilininda na Madilu wilayani humo.

Thomas amesema fedha hizo zimetolewa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuleta mapinduzi katika sekta ya afya.

Ameeleza kuwa mradi huo mpya hautahusisha kumalizia majengo ya zamani, bali utaanza na ujenzi wa majengo mapya ya kisasa.

“Nawaomba wananchi wa Madilu kuupokea mradi huu kwa mikono miwili. Ni mradi wenu, serikali imesikia kilio chenu. Nawapongeza kwa hatua mliyofikia kwa kujitolea kuanza ujenzi kwa nguvu zenu wenyewe; mmeonesha moyo wa uzalendo na dhamira ya kweli ya maendeleo,” amesema Mkuu huyo wa Wilaya.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo hilo, Joseph Kamonga, ambaye aliambatana na Mkuu huyo wa Wilaya, amesema amekuwa mstari wa mbele kupigania upatikanaji wa kituo cha afya katika Kata ya Madilu kutokana na mazingira ya kijiografia ya eneo hilo, ambayo yamekuwa kikwazo kwa wananchi kupata huduma bora za afya.

Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Dk. Twilumba Lihweuli, amesema kituo hicho kitakuwa cha kisasa na kitaambatana na majengo muhimu ikiwemo jengo la wagonjwa wa nje (OPD) lenye vyumba vya madaktari, maabara, mapokezi na sehemu za mapumziko ya muda mfupi, jengo la upasuaji, jengo la kuchomea taka, kufulia pamoja na miundombinu mingine muhimu.

Ujenzi wa kituo hicho cha afya unatarajiwa kuleta afueni kwa wakazi wa Kata ya Madilu na vijiji jirani ambao kwa muda mrefu wamekumbana na changamoto ya kupata huduma za afya karibu na maeneo yao.