Maaskofu na Wachungaji wanaohudumu katika Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Mkuu Josephat Gwajima wamefika Makao Makuu ya Ofisi za Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania(THRDC) kuomba msaada wa kisheria katika sakata la kufungiwa makanisa hayo nchi nzima.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam mbele ya vyombo vya habari kwa niaba ya maaskofu hao Askofu Amos Paul kutoka Mkoa wa Shinyanga alisema wamekuja THRDC ili waweze kupata msaada wa kisheria dhidi ya mgogoro huo dhidi ya Serikali kufungiwa makanisa hayo huku wakiwa katika sintofahamu ya haki yao ya kuabudu.
Alisema wamefika THRDC kwa kuamini ni taasisi kubwa na nyeti inayoaminika ndani na nje ya nchi ambayo inajihusisha na utetezi wa haki za binadamu wawatetee ili waweze kupata haki yao ya kimsingi ya kuabudu.
“Tumekuja hapa kudai haki yetu ya kimsingi ya kuabudu, tukiamini THRDC watatusaidia kwa asilimia 100, tunaiomba Serikali isikie kilio cha wananchi wake ambao kwa sasa wako njiapanda wanakosa haki ya kuabudu” alisema
Aidha alifafanua kuwa kufungiwa kwa makanisa hayo nchi nzima kumefanya kukosekane kwa ajira zaidi ya elfu sita (6000) nchi nzima ambao wanategemewa na familia zao kwa ajira hizo, ambao kati ya waliopoteza ajira wakiwemo maaskofu, wasaidizi wa maaskofu, wahasibu na wahudumu wengine.
Alifafanua Serikali inatakiwa itambue ya kuwa waumini wa makanisa hayo ni ngumu kuwahamisha wakaabudu kwenye makanisa mengine kwa kuwa imani zao zipo katika kuabudu makanisa za ufufuo na uzima na hakutakuwa na mbadala juu ya kuwafanya kuwaamisha imani..
“Makanisa yetu hayajafungwa tu bali yalivamiwa na kuvunjwa huku waumini wakipigwa hivyo hadi sasa tuna hofu kubwa kwakuwa hata kama makanisa yakifunguliwa hatujui tutakuta hali gani ndani ya makanisa hayo kwakuwa ndani ya makanisa kuna mali nyingi yakiwemo masanduku ya kuhifadhia pesa za sadaka, vyeti vya ndoa, nyaraka mbalimbali na mali nyingine nyingi za kanisa” alisema
Kwaupande wake Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Onesmo Olengurumwa alimtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, IGP na Kamanda Jeshi la Polisi watafute namna ya kukutana na maaskofu na viongozi hao waweze kukaa mezani kulizungumza suala hilo kwa kina kwa utaratibu wa kusikilizana.
Alisema wakichukua hatua hiyo ni vyema zaidi kwakuwa watafikia muafaka mzuri hata wa kuwaachia waabudu huku wakiendelea kumshikilia kiongozi mkuu wa kanisa hilo Askofu Gwajima huku taratibu zingine zikiendelea.
Alisema itakuwa vyema na utu endapo Jeshi la Polisi watawaruhusu waumini wa makanisa hayo wafanye ibada hata katika viwanja vingine kwani kuendelea kuwazuia ni kinyume na uvunjifu wa haki za binadamu.
“Kuwazuia watu wasifanye ibada ni kosa na kinyume na uvunjifu wa haki za binadamu kwakuwa hata Katiba ya nchi inasema kila mmoja ana haki ya kuabudu kokote atakapo hivyo wahusika waliangalie hili, sisi kama watetezi kama endapo waumini hawa wataendelea kuzuiliwa kuabudu basi tutachukua hatua zingine kwakuwa kazi yetu ni kutatua migogoro katika jamii” alisema
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED