Samia amwaga fedha lami Mpwapwa-Kongwa- Mbande

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 07:13 PM Jun 23 2025

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Mpwapwa-Kongwa- Mbande itakayojengwa kwa kiwango cha lami.

Ameyasema hayo leo Juni 23, 2025, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mpwapwa mjini, mkoani Dodoma, wakati wa ziara yake ya siku tatu aliyoianza ikihusisha Dodoma na Singida.

Amesema tayari Rais Samia ameshatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo,ambapo kwa sasa mkandarasi ameanza maandalizi yake.

Makalla amesema Rais Samia ameshusha mabilioni ya fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali, akiwaeleza wananchi kwamba, maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Kongwa- Mpwapwa mkandarasi yuko kwenye maandalizi na ya Kibakwe manunuzi kwa ajili kujengwa yanaendelea.

“Ukiwasikiliza wabunge na Mkuu wa Wilaya wameeleza miradi mbalimbali iliyotekelezwa, ningemwambia (Job) Ndugai (mbunge wa Kongwa) aseme habari ya Kongwa tungekesha, kila mahali kuna alama ya maendeleo yaliyofanywa na serikali.

“Kuna wananchi wameshuhudia shule zikijengea, elimu bila malipo, vituo vya afya, umeme vijijini, madaraja yakijengwa, mambo ni mengi yaliyofanywa na hayo yamesababisha wananchi kwa kauli moja katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kukiamini CCM, yote yamefanywa chini ya Rais Samia,” amesema.

Mbunge wa  Mpwapwa, George Malima, ametaja miradi mbalimbali iliyotekelezwa katika kila sekta ya afya, elimu na maji, huku akieleza baadhi ya changamoto zilizobaki ikiwamo barabara Kongwa- Mpwapwa ya Sh.  bilioni 51.

“Changamoto nyingine ni daraja godegode ambapo mkandarasi ameshapatikana, tuna changamoto ya vituo vya afya tunaamini kata za kimkakati baada ya muda mfupi zitapata huduma hizo,” amesema.