“Wanasiasa wana wajibu wa kulinda mema ya jamii, kukuza uhuru wa kidini na kukabiliana na changamoto kubwa ya Akili Bandia (AI), hasa kwa ajili ya mustakabali wa vijana,” amesema Papa Leo XIV.
Baba Mtakatifu aliyasema hayo mbele ya wabunge 600 kutoka nchi 68 duniani, katika hafla ya Jubilei ya Watawala wa Serikali na Taasisi za Kiraia, iliyofanyika Jumamosi, Juni 21, 2025, katika Ukumbi wa Baraka, Vatican.
Akiwahutubia viongozi hao, Papa Leo alisisitiza kuwa siasa si taaluma, bali ni wito wa kutumikia ukweli na wema kwa manufaa ya wote. Alitoa mfano wa Mtakatifu Thomas More, ambaye alisimamia uhuru wa dhamiri hadi kufikia kufa shahidi.
Katika hotuba yake, Papa alisisitiza mambo matatu muhimu kwa wanasiasa: kwanza, kulinda maslahi ya jamii kwa kuwajali wanyonge na waliotengwa; pili, kuhakikisha uhuru wa kidini na kuhimiza mazungumzo ya kidini; na tatu, kushughulikia changamoto ya Akili Bandia (AI) kwa kuzingatia afya, haki na usalama wa vijana.
Akitolea mfano wa hali ya sasa duniani, Papa alionya juu ya tofauti kubwa kati ya matajiri wachache na umati wa maskini, akisema hali hiyo inazalisha ukosefu wa haki na machafuko, na kwamba siasa nzuri inaweza kuwa daraja la amani ya ndani na kimataifa.
Kuhusu uhuru wa kidini, Baba Mtakatifu alieleza kuwa imani katika Mungu huleta maadili chanya kwa jamii. Alinukuu mafundisho ya Mtakatifu Agostino kuhusu umuhimu wa kupita kutoka upendo binafsi kuelekea upendo wa kweli kwa Mungu, jambo ambalo linaimarisha mshikamano katika jamii.
“Tunapozungumzia siasa, tunazungumzia tendo la juu la upendo kwa jamii,” alisisitiza Papa, akinukuu pia maneno ya Papa Pio XI.
Kwa kumalizia, alitoa wito kwa wanasiasa kuwa mstari wa mbele kuondoa ukosefu wa usawa, kuhimiza mazungumzo ya kidini, na kushirikiana kwa ajili ya mustakabali wa kizazi kijacho.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED