Nchi nane za Afrika zimekutana mkoani Mtwara kwa mafunzo ya siku tano yanayolenga kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao la korosho – kuanzia uzalishaji, ubanguaji, uongezaji wa thamani, masuala ya sera, mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na ushindani wa zao hilo barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Mafunzo hayo, yanayoendeshwa chini ya usimamizi wa African Cashew Alliance (ACA), yamefunguliwa rasmi leo na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, ambaye alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kwa kazi kubwa ya kusimamia sekta ya kilimo, pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuweka msukumo mkubwa katika kuendeleza zao la korosho nchini.
“Rais wetu ameendelea kuimarisha sekta ya kilimo kwa kutoa pembejeo bure, kuongeza ajira kwa maafisa ugani, pamoja na kuhakikisha masoko ya uhakika kwa wakulima. Tunamshukuru kwa moyo wake kwa wakulima wa Tanzania,” alisema Kanali Sawala.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Alfred Francis, alisema kuwa Tanzania kwa sasa inashika nafasi ya tano duniani kwa uzalishaji wa korosho na ya pili barani Afrika, nyuma ya Ivory Coast.
“Mafunzo haya ni muhimu sana kwa Tanzania kwa kuwa tunatekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha mnyororo mzima wa korosho. Tunajenga kongani la viwanda vya ubanguaji korosho na maghala Maranje, na tayari tumeajiri zaidi ya maafisa ugani 500. Mafunzo haya yatatusaidia kuongeza tija na ushindani wa zao letu,” alisema Alfred.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dkt. Sophia Kashenge, alisema korosho ni zao lenye mchango mkubwa kiuchumi na kijamii nchini, lakini changamoto za mabadiliko ya tabia nchi na kupungua kwa rutuba ya ardhi zimekuwa zikikwamisha uzalishaji.
“Idadi ya watu inaongezeka lakini ardhi yenye rutuba inapungua. Hii ni changamoto ambayo hatuwezi kuikwepa peke yetu, tunahitaji ushirikiano wa kitaifa na kimataifa ili kusaidia mkulima kuongeza uzalishaji wake,” alisema Dk. Kashenge.
Katika hatua nyingine, imetangazwa kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa 19 wa mwaka na Maonesho ya Zao la Korosho kwa nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (ACP) yatakayofanyika Novemba 18 hadi 22, 2025, ambapo kaulimbiu ya mwaka huu itakuwa “Wekeza kwenye korosho kwa maendeleo endelevu.”
Nchi zinazoshiriki mafunzo hayo ni Tanzania, Kenya, Ghana, Sudan Kusini, Msumbiji, Uganda, Rwanda na Zambia. Mafunzo hayo yanatarajiwa kusaidia nchi wanachama kubadilishana uzoefu na kuunda mikakati ya pamoja ya kuongeza tija, thamani na soko la zao la korosho ndani na nje ya Afrika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED