Waziri wa Maliasili na Utalii,Balozi Dk. Pindi Chana ameelekeza kujengwa kwa maabara za kupima ubora wa asali nchi nzima sambamba na kufanya tathmini muundo wa kada ya ufugaji nyuki kwa lengo la kuikuza Sekta ya Ufugaji Nyuki.
Ameyasema hayo katika kikao cha 17 cha kamati ya Taifa ya Ushauri ya Maendeleo ya ufugaji nyuki (NABAC) kilichofanyika leo Juni 23, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Taifa cha Utalii jijini, Dar es salaam
“Tayari tuna maabara ya mazao ya nyuki iliyopo Njiro, hizi maabara tunahitaji nyingi za kutosha ili zihudumie Tanzania nzima hivyo tuangalie namna gani kila mkoa uwe na maabara” amesisitiza Chana.
Aidha amesema wakati umefika wa kuangalia kwa ukaribu kada ya ufugaji kuona namna gani wanaweza kuboreshewa mshahara na maslahi mengine na kuhakikisha kunakuwa na vikao vya mara kwa mara kusikiliza changamoto zao na mawazo ya kuikuza sekta hiyo.
“Naelekeza tuwe na kikao cha maafisa nyuki Tanzania nzima kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI tupate mawazo yao kwa sababu ajira zao zimekuwa changamoto” amesema Chana.
Aidha,Chana ameipongeza kamati hiyo kwa mafanikio iliyoyapata katika Wizara ya Maliasili na Utalii baada ya kumaliza muda wake wa kuhudumu kwa mujibu wa sharia kwa kipindi cha miaka mitatu.
“Kuhusu uimarishaji wa maeneo ya kufugia nyuki kwa kutenga na kuanzisha hifadhi za nyuki mathalani, ndani ya kipindi cha miaka mitatu jumla ya hifadhi za nyuki 13 zimeanzishwa na hifadhi za nyuki 23 zipo katika hatua mbalimbali za kukamilisha taratibu za kuzitangaza” amesem Chana.
Ameongeza kuwa kamati hiyo imewezesha kuongezeka kwa mauzo ya nyuki katika masoko ya ndani na nje ya nchi hivyo kuwezeshwa kuanzisha Alama ya Asali ya Tanzania, pamoja na kufungua masoko mapya ya asali katika nchi za Umoja wa Ulaya, Asia, na China;
Chana amesema kupitia kamati hiyo pia kumewezeshwa kuanzishwa kwa programu za kuendeleza ufugaji nyuki ambapo Wizara kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya imefanikiwa kutekeleza programu ya kuwezesha mnyororo wa ufugaji nyuki, pamoja na kuandaa Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Ufugaji Nyuki kwa Tanzania Iliyo Bora ambayo itaanza kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha.
Pia ili kuikuza sekta ya ufugaji nyuki Chana ameelekeza kutoa mafunzo kwa mafundi seremala kote nchini ili waweze kutengeneza mizinga ya nyuki ya kisasa , TFS kuangalia uwezekano wa kuweka vituo vya kununulia asali nzima.
Kuangalia uwezekano wa kuwa na maabara ya kupimia ubora wa asali katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwarahisishia wafanyabiashara kupata huduma kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya NABAC, Jackson Msome ameipongeza Serikali chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan Sekta ya Ufugaji Nyuki imeendelea kukua na imetambulika rasmi.
Amesema katika kipindi cha miaka mitatu (2022/23 – 2024/25) kamati imewezesha kuandaliwa na kuzinduliwa kwa Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Ufugaji nyuki Tanzania (Achia Shoka, Tundika Mzinga), Tanzania kushinda nafasi ya kuwa mwenyeji wa (APIMONDIA) 2027 na Tanzania kupata soko la asali nchini China (Tani 38,000).
Pia amesema kamati hiyo imewezesha Tanzania kupata nembo ya asali itakayotumika kuitangaza asali katika soko la ndani na nje ya nchi pamoja na kutolewa kwa msahama wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye baadhi ya vifaa muhimu kwenye uchakataji wa mazao ya nyuki.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Wizara ya Maliasili na Utalii (MNRT) Bernard Marcelline, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Wizara ya Maliasili na Utalii, Abdallah Mvungi , Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Deusdedith Bwoyo pamoja na baadhi ya Wakurugenzi Wasaidizi na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED