Makalla: Tumesitisha mikutano kupata utulivu wa kutafakari wagombea

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 07:33 PM Jun 24 2025
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla

Baada ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) kusitisha kwa muda mikutano, ziara na makongamano, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla, amesema ni muhimu kufanya hivyo ili wakajipange na maandalizi ya kura za maoni na kupata utulivu kutafakari wagombea.

Jana, Katibu Mkuu CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, kupitia taarifa yake aliyotoa, alitangaza kuhusu kusitisha kwa muda shughuli hizo.

Akizungumza leo Juni  24, 2025, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Dodoma mjini, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya siku tatu, Makalla amesema ni sahihi maelekezo yaliyotolewa.

“Nimesimama hapa kuwaeleza tutasimama kwa muda kwa maandalizi ya kura za maoni ndani ya chama.

“Mabalozi ni watu muhimu ndio wako kule ndio wana wanachama, tuwape nafasi kuandaa mazingira kuelekea kura za maoni,viongozi wa matawi, kamati za siasa za matawi, kata, wilaya, mkoa na wenyewe wapate nafasi ya kujiandaa kuratibu kura za maoni.

“Muda hauko upande wetu, tunasitisha ziara hizi ili kutoa nafasi ya maandalizi ya mchakato ndani ya chama chetu. Maana hawa tukiwa tunawaita mara kwa mara watakosa muda wa kufanya maandalizi.