Tarimba:Nitaendelea kupambana na wanaomtingisha Rais Samia

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 02:07 PM Jun 24 2025
Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba.

Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba, amesema yuko tayari kuitwa majina yote kwa kusema mazuri yote yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema tangu Rais Samia aingie madarakani amefanya mambo mengi makubwa na kwamba ndiyo sababu ambayo imekuwa ikimsukuma apambane na yeyote ambaye alionekana kumsema vibaya kiongozi huyo wa nchi.

"Ndiyo maana nilijitosa, nikasema atakayemtingisha Rais nami nitamtingisha, bila shaka nimekuwa nikifanya hivyo ndani na nje ya bunge.


"Malipo pekee tunayotakiwa kwenda kumlipa Rais wetu ni kusubiri Oktoba twende tukatiki ili ashinde kwa kishindo na aendelee kutuhudumia na kutueletea Maendeleo kwenye maeneo yetu,"alisema Tarimba.


Kadhalika, Tarimba alisema katika kipindi cha miaka mitano kwenye jimbo lake mambo mengi yamefanyika ikiwamo kujenga vituo vya afya, kuboresha miundombinu ya barabara na katika sekta ya elimu kupitia mfuko wa jimbo. 

Pia, alisema yeye binafsi amejitolea kuchangia kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo kwenye sekta ya elimu na maeneo mengine. 

Eneo jingine alisema alijitolea kutoa bima ya afya kwa wananchi wake zaidi 1300 na kwamba hilo litaendelea kufanyika.

"Huu ni mpango ambao niliubuni miaka mingi nikiamini kwamba watu wetu wanahitaji afya bora ili waendeshe shughuli zao kwa urahisi, nilifanya hivyo na nitaendelea kusaidia katika eneo hilo,"alisema Tarimba.


Tarimba alisema yuko tayari kutetea jimbo hilo kwa mara nyingine wakati ukifika.