Wanachama 280 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na ACT Wazalendo mkoani Dodoma wakiwamo madiwani watatu wametangaza kutimkia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akiwapokea wanachama hao leo Juni 24, 2025, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Dodoma mjini, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla, amesema jeshi hilo litaongeza nguvu CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Amesema wanachama wa CHADEMA wanahama kwa kuwa viongozi wao wamefanya uamuzi ambao haukuwafurahisha wanachama wao.
Makalla amesema kwa sasa CCM kina wanachama milioni 13, na kwa idadi hiyo waliyopokea wanakwenda kuongeza nguvu na chachu ya kusaka kura za CCM katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Kadhalika, amesema mkoa huo una historia ya majimbo yote kuwa CCM, ambapo kwa takwimu zilizotolewa zinadhibitisha vijiji vingi, vitongoji, kata ni ngome yao.
“Wana Dodoma kwa kuendelea kuwa ngome ya CCM mnakiheshimisha Chama Cha Mapinduzi na nchi kwamba, nyie ni Makao Makuu na Makao Makuu ya chama yako hapa,” amesema.
Diwani wa Kigwe kupitia ACT Wazalendo, Adon Mabalwe, aliyetangaza kuhamia CCM, alipopewa nafasi ya kuzungumza katika mkutano huo, amesema wameamua kurudi nyumbani kwa sababu kumenoga.
“Miaka mitano tuliyokaa nje ya CCM tumejifunza mengi, tumekuja kuungana na wenzetu CCM isonge mbele,” amesema.
Madiwani wengine wa ACT Wazalendo waliorudi CCM ni kutoka Chamwino na Chemba.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED